Seneta Miraj Abdillahi Apongeza juhudi za serikali katika Kupambana na Mihadarati Mombasa.
Seneta Mteule katika kaunti ya Mombasa Miraj Abdillahi amepongeza idara za usalama kwa juhudi zake za kupambana na matumizi ya mihadarati pamoja na kuimarisha usalama katika Kaunti ya Mombasa, hatua ambayo amesema imechangia kupungua kwa visa vya uhalifu na utovu wa usalama vilivyokuwa vikishuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo. Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya usalama na wananchi. Akizungumza katika eneo bunge la Jomvu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Miraj amesema ukanda wa Pwani kwa miaka mingi umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya matumizi na biashara ya mihadarati. Hata hivyo, amebainisha kuwa kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Usalama wa Ndani, vyombo vya usalama na serikali ya kaunti, hatua kubwa zimepigwa katika kudhibiti tatizo hilo. Amesema juhudi hizo zimewaokoa vijana wengi kutoka katika uraibu wa dawa za kulevya na kuwapa fursa ya kujijenga upya na kuboresha maisha yao....