Wito wa Ushirikiano Watolewa Katika Vita Dhidi ya Mihadarati Nchini.



                               

Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya kupinga matumizi na ulanguzi wa dawa za kulevya,hapa Mombasa siku hiyo imeadhimishwa katika eneo bunge la Jomvu katika kituo cha Miritini huku viongozi wakionya kuwa taifa linakabiliwa na dharura ya kitaifa kutokana na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya,wito ukitolewa kwa serikali za kaunti pamoja na serikali ya kitaifa kushirikiana kwa karibu ili kuimarisha vita dhidi ya mihadarati .

Kulingana na utafiti wa hivi karibuni wa kitaifa uliofanywa na Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA), takriban Wakenya milioni 4.7 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 65 wanatumia angalau aina moja ya dawa za kulevya au kilevi.

Utafiti huo unaonyesha kuwa eneo la Pwani lina kiwango cha juu zaidi cha matumizi ya dawa za kulevya nchini kwa asilimia 29.3, huku Kaunti ya Mombasa ikiongoza kwa kiwango cha asilimia 34.4.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi Mabaya ya Dawa za Kulevya na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya (IDADA) 2026, Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Dkt. Raymond Omollo, amesema Kenya inashuhudia mwelekeo mpya wa dawa za kulevya, ikiwemo kuanza kutengenezwa kwa dawa za kisasa ndani ya nchi.

                                         

Dkt. Omollo amesema kuwa ingawa mamlaka zimekuwa zikijikita katika kupambana na matumizi ya bangi na pombe, sasa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanatumia teknolojia kuzalisha dawa za kisasa nchini, jambo linalofanya iwe vigumu kuzibaini.

Katibu huyo Mkuu ameonya kuwa eneo la Pwani linaendelea kuwa kitovu kinachovutia wasafirishaji wa kimataifa wa dawa za kulevya kutokana na nafasi yake ya kijiografia, akiongeza kuwa magenge ya uhalifu yanatumia teknolojia ya kisasa na mitandao ya kimataifa kusafirisha dawa hizo haramu.

Amefichua kuwa mwaka uliopita vyombo vya usalama vilinasa dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi bilioni 8.2, akisema huo ni miongoni mwa ukamataji mkubwa zaidi wa dawa za kulevya kuwahi kufanywa nchini.

                                       

Aidha, amewataka wazazi,taasisi za elimu, taasisi za kidini, mashirika ya kijamii na sekta binafsi kushirikiana kuimarisha juhudi za kuzuia matumizi ya dawa za kulevya, kutoa huduma za mapema, matibabu na urekebishaji wa waraibu ili kukabiliana na tatizo hilo.

Mkurugenzi mkuu wa NACADA Anthony Omerikwa amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya serikali ya kitaifa, serikali za kaunti na jamii kwa ujumla.

 Ametoa wito wa kuimarishwa kwa kampeni za uhamasishaji katika jamii, shule na maeneo ya kazi ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya pombe na dawa za kulevya, akisisitiza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha vijana wanaokolewa kabla hawajapoteza kabisa mwelekeo wa maisha yao.

                                     

Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Sharif Nassir, ameahidi kuimarisha ushirikiano na taasisi pamoja na mashirika yanayopambana na mihadarati ili kuokoa maisha ya vijana.

Gavana Nassir ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na vileo haramu.

Amesema kuwa kupitia mazungumzo na mashauriano aliyofanya hivi karibuni na viongozi mbalimbali, imebainika kuwa vileo haramu vinauzwa kwa bei nafuu, jambo linalochochea matumizi yake na kuathiri maisha ya vijana wengi katika kaunti hiyo.

                                 

Nae seneta mteule katika kaunti ya Mombasa Miraj Abdillah  amesema ukanda wa Pwani kwa miaka mingi umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya matumizi na biashara ya mihadarati.

Akibainisha kuwa kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Usalama wa Ndani, vyombo vya usalama na serikali ya kaunti, hatua kubwa zimepigwa katika kudhibiti tatizo hilo. Amesema juhudi hizo zimewaokoa vijana wengi kutoka katika uraibu wa dawa za kulevya na kuwapa fursa ya kujijenga upya na kuboresha maisha yao.


Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.