Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.
Kaunti ya Wajir imeandika historia kwa kuandaa sherehe za 63 za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate uhuru. Serikali imesema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kuhakikisha maendeleo na shughuli za kitaifa zinafikia maeneo yote ya nchi huku zikikuza umoja, usawa na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea maadhimisho hayo, Msemaji wa Serikali, Isaac Mwaura, amesema kuwa tukio hilo linaonyesha dhamira ya serikali katika kukuza ushirikishwaji, usawa na mshikamano wa kitaifa.
Alibainisha kuwa licha ya
changamoto za uchumi wa dunia, ikiwemo athari za mgogoro unaoendelea Mashariki
ya Kati, uchumi wa Kenya umeendelea kuwa thabiti na hivyo kuwezesha serikali
kuendelea kuwekeza katika maendeleo na umoja wa kitaifa.
Maandalizi ya sherehe hizo yameleta mabadiliko makubwa katika mji wa Wajir, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 10,000, uboreshaji wa barabara, uwekaji wa taa za kisasa za barabarani na ujenzi wa mini State Lodge.
Miradi hiyo inatarajiwa kuboresha huduma na kuongeza uwezo wa eneo hilo kuandaa shughuli za kitaifa siku zijazo.
Wakati huo huo, serikali inaendelea kutekeleza karibu miradi 30 ya maendeleo katika kaunti za Wajir, Garissa na Mandera.
Miradi hiyo inajumuisha masoko ya kisasa, maktaba, vituo vya wanafunzi, nyumba nafuu pamoja na miradi ya barabara, maji na usafi wa mazingira.
Serikali
inasema uwekezaji huo utachochea ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma za jamii na
kuunda nafasi za ajira kwa wakazi wa eneo hilo.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu ya “Elimu, Ujuzi na Mustakabali,” ikisisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kupitia elimu bora na mafunzo ya ufundi.
Zaidi ya madarasa 1,000 pamoja na
miradi mingine ya elimu inaendelea kujengwa huku maonyesho ya elimu na
teknolojia katika Wagberi Primary School yakionyesha juhudi za serikali za
kuandaa vijana kwa fursa za uchumi wa kisasa.
Viongozi wamewataka Wakenya kuendelea kudumisha amani, umoja na uzalendo huku wakishiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Wamesema maadhimisho ya mwaka huu si tu kumbukumbu ya safari ya Kenya kuelekea
kujitawala, bali pia fursa ya kutafakari kuhusu mustakabali wa nchi unaojengwa
kupitia elimu, ubunifu na maendeleo jumuishi.
Viongozi mbalimbali kutoka nchini nan je ya nchi
wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hizo.





Comments
Post a Comment