Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula Akemea Siasa za Ukabila na Vurugu.

                                                                

                                          

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang'ula, amewataka Wakenya kujiepusha na siasa za ukabila na kukumbatia umoja wa kitaifa, akisema mustakabali wa nchi unategemea viongozi na wananchi kuweka maslahi ya taifa mbele badala ya tofauti za kikabila na kisiasa.

Akizungumza katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, wakati wa hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Shirika la Kijamii la Salute (Salute CBO), Wetang'ula amesema maendeleo ya Kenya yatawezekana kupitia umoja, mshikamano na kuheshimu demokrasia.

"Nchi yetu ni kubwa kuliko mtu yeyote, na uongozi hutoka kwa Mungu. Lengo letu linapaswa kuwa kuunganisha taifa tunapoendelea kuelekea kuwa nchi yenye maendeleo makubwa," alisema.

                                       

Amesisitiza kuwa hakuna jamii iliyo kubwa au ndogo nchini Kenya na kwamba kila jamii ina haki ya kutoa viongozi wake. Aidha, alitoa wito kwa wanasiasa kudumisha siasa za heshima kwa kushindana kwa amani wakati wa uchaguzi na kukubali matokeo baada ya uchaguzi.

"Hakuna kabila kubwa wala dogo nchini Kenya. Kila jamii ina haki ya kuongoza taifa hili. Tunapaswa kudumisha siasa zenye staha ambapo tunashindana kwa nguvu wakati wa uchaguzi, lakini matokeo yanapotangazwa, tunakumbatiana na kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya wote," alisema.

                                       

Spika huyo pia amekemea tabia inayoshuhudiwa ambapo baadhi ya wanasiasa wanadaiwa kudhamini na kutumia makundi ya wahuni kusababisha vurugu za kisiasa, akionya kuwa hali hiyo inahatarisha amani na utulivu uliopatikana kwa juhudi kubwa.

"Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wanasiasa wakiajiri wahuni kuvuruga amani yetu tuliyoijenga kwa gharama kubwa. Tunapaswa kukemea vitendo hivyo. Ikiwa wanahitaji wahuni, waajiri watoto wao wenyewe, si watoto wasio na hatia wa taifa hili," alisema.

Wetang'ula amempongeza aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kuweka maslahi ya taifa mbele baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, akisema hatua hiyo ilichangia kuundwa kwa serikali jumuishi inayowapa viongozi kutoka pande mbalimbali za kisiasa nafasi ya kuhudumia taifa.

Wetangula pia ameeleza matumaini yake kuhusu mustakabali wa Kenya, akisema nchi iko katika mkondo wa ukuaji endelevu na ustawi wa kiuchumi. Akisema utawala wa Rais William Ruto umeweka msingi wa mageuzi ya kiuchumi huku taasisi za kidemokrasia zikiendelea kuimarika.

                                     

Naye Spika wa Seneti, Amason Kingi, ameunga mkono wito wa kukomeshwa kwa siasa za ukabila, akisema eneo la Pwani ni la watu wa tamaduni mbalimbali na haliwezi kuunga mkono siasa za mgawanyiko wa kikabila.

"Pwani ni eneo lenye watu wa asili na tamaduni tofauti. Hilo pekee linatupa sababu ya kuunga mkono serikali jumuishi. Kenya imepiga hatua kubwa katika kuondoa mfumo wa kale wa kuwagawa wananchi kwa misingi ya ukabila," alisema.

                                    

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Hassan Joho alimshukuru Rais William Ruto kwa kuhakikisha Wakenya wote wanatendewa maendeleo  kwa usawa bila kujali kabila wala dini.

"Kwa miaka mingi, watu wetu walipuuzwa kiuchumi na kisiasa. Kwa mara ya kwanza, tumesimama kidete na kukubaliana kwamba sisi pia tunaweza kuongoza. Huu ni wakati wetu wa kuifanya Kenya kuwa taifa bora zaidi," alisema.

                                         

Mbunge wa Likoni, Mishi Mboko, alimshukuru Wetang'ula kwa ushauri na uongozi wake, akisema atarudisha wema huo kwa wakati unaofaa.

"Sisi ni matokeo ya malezi na mwongozo bora. Tumeazimia kwamba wakati utakapofika, nasi tutawaunga mkono wale waliotunyanyua. Kwa pamoja tunaamini kuwa taifa letu liko kwenye njia sahihi kuelekea ustawi," alisema.

                                         

 


Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.