Maadhimisho ya Siku ya Mtoto mwafrika: Viongozi Kilifi watoa Wito wa Kulinda Watoto.

 

                                                      

Viongozi wa Kaunti ya Kilifi wametoa wito kwa jamii kushirikiana katika kuimarisha ulinzi wa watoto na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu, huduma za afya, maji safi na mazingira salama ya kuishi.

Wakizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa mwafrika, viongozi hao walisisitiza kuwa jukumu la kulinda watoto si la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwanajamii.

                                                         

Akiongea katika hafla hiyo naibu Gavana wa Kilifi, Flora Chibule, amesema maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kutafakari wajibu wa pamoja wa kulinda, kulea na kuwekeza kwa kila mtoto ili kuhakikisha anafikia ndoto zake.

Akiangazia kaulimbiu ya mwaka huu, “Kuhakikisha Kila Mtoto wa mwafrika Anapata Huduma ya Maji Safi, Usafi wa Mazingira na Afya ya Usafi,” Chibule amesema upatikanaji wa maji safi ni haki ya msingi inayostahili heshima na utu.

                                             

Alieleza kuwa ukosefu wa maji safi na huduma bora za usafi wa mazingira huwanyima watoto muda wa kujifunza na kuwaweka katika hatari ya maradhi, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia wanapolazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Chibule ameonya kuwa changamoto kama biashara haramu ya watoto, unyanyasaji wa kijinsia, mimba za utotoni, mila potofu, umaskini na migogoro ya kifamilia zinaendelea kuhatarisha ustawi wa watoto katika kaunti hiyo.

“Mtoto wa mwenzako ni mtoto wako. Ulinzi wa mtoto huanza pale jamii inapochukua hatua za kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto wote,” alisema.

Kwa upande wake, Afisa wa Watoto wa Kaunti ya Kilifi, Kelvin Mugambi, aliwataka wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kuripoti kwa wakati visa vyote vya dhuluma na unyanyasaji dhidi ya watoto ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

                                                   

Mugambi amesema serikali ya kitaifa na ile ya kaunti zinapaswa kuendelea kuwekeza katika mazingira salama kwa watoto pamoja na kushughulikia changamoto za upatikanaji wa maji katika maeneo yenye ukame ili watoto wapate fursa ya kuhudhuria masomo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Naye Waziri wa Vijana, Michezo na Huduma za Jamii, Dr Ruth Dama Masha, aliwataka wazazi na walezi kuimarisha mawasiliano na watoto wao na kuwapa ushauri nasaha ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo afya ya akili na msongo wa mawazo.

                                                      

Ruth pia aliwahimiza watoto kujiepusha na matumizi ya mihadarati, akisema kuwa yana madhara makubwa kwa afya na yanaweza kuharibu ndoto na mustakabali wa maisha yao.

Viongozi hao walisisitiza kuwa Serikali ya Kaunti ya Kilifi itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto, hususan wale wanaoishi na ulemavu, na kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa za kutimiza ndoto zao.





Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.