Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Yawapa Walemavu Mafunzo ya Masuala ya Uchaguzi.


                                                             
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa nchini imeandaa mafunzo maalum ya maandalizi ya uchaguzi kwa walemavu katika Kaunti ya Mombasa, yakilenga kuwajenga uwezo, kuwafahamisha haki zao na kuongeza ushiriki wao katika mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mratibu kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa katika kaunti ya Mombasa Suzan Mwaingo amesema lengo kuu ni kuwahamasisha walemavu kujiunga na vyama vya kisiasa na kufahamu namna wanavyoweza kupata nafasi za uongozi kupitia uteuzi wa vyama.

Akisema ofisi hiyo imejipanga vyema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 na imeendelea kushirikiana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutoa elimu kuhusu sheria za uchaguzi na umuhimu wa kuzingatia sheria hizo ili kuepuka adhabu.

Suzan amebainisha kuwa vyama 48 kati ya 96 vilivyosajiliwa nchini vimekidhi vigezo vya kupokea fedha kutoka Mfuko wa Vyama vya Kisiasa unaolenga kuunga mkono makundi maalum, wakiwemo walemavu. 

                                                 

Aliwahimiza walemavu kujiunga na vyama vya kisiasa ili waweze kunufaika na fursa na rasilimali zinazotolewa kupitia mfuko huo.

Kwa upande wake, msimamizi wa data katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa,Josphat  Nyongesa, amesema mafunzo hayo yanaonyesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha ushiriki jumuishi katika uchaguzi na siasa.

Amesisitiza kuwa walemavu wana haki ya kushiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia, ikiwemo kupiga kura, kuwania nyadhifa za kisiasa na kushiriki katika maamuzi ya kitaifa.

Nyongesa amesema matumizi ya teknolojia yamekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha ushiriki wa walemavu kupitia vifaa saidizi, majukwaa ya kidijitali na mitandao ya kijamii. Akiweka wazi kuwa teknolojia imechangia kurahisisha upatikanaji wa huduma na taarifa za uchaguzi kwa walemavu.

Amewataka walemavu kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya ili kupata taarifa sahihi, kutetea haki zao, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushiriki wao katika masuala ya demokrasia.

                                               

Maafisa hao pia wamesisitiza umuhimu wa vyama vya kisiasa kuzingatia sheria na kuhakikisha walemavu wanapata haki zao, hasa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Jemyma Kutata, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuelewa haki zao na namna wanavyoweza kunufaika kupitia vyama vya kisiasa.

Ameitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kuhakikisha sheria zinazowalinda walemavu zinatekelezwa kikamilifu ili waweze kufaidika na fursa zilizopo.

Akiwahimiza walemavu kujitokeza kuwania nafasi za uongozi kupitia uchaguzi badala ya kusubiri uteuzi, akisema wana uwezo wa kushindania na kushinda nyadhifa mbalimbali za kisiasa.

Aidha, ameiomba IEBC kutenga huduma na maeneo maalum kwa watu wenye ulemavu wakati wa usajili wa wapiga kura na siku ya kupiga kura ili kuepusha changamoto za kupanga foleni, ambazo mara nyingi huwasababishia usumbufu na kuwafanya wajihisi kutengwa.

                                             

Pia ameitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kushirikiana kwa karibu na time ya IEBC ili kuhakikisha walemavu wanapata haki yao katika uteuzi wa vyama vya kisiasa, badala ya nafasi hizo kutolewa kwa watu wasio na ulemavu.

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.