Seneta Miraj Abdillahi Apongeza juhudi za serikali katika Kupambana na Mihadarati Mombasa.

 


Seneta Mteule katika kaunti ya Mombasa Miraj Abdillahi amepongeza idara za usalama kwa juhudi zake za kupambana na matumizi ya mihadarati pamoja na kuimarisha usalama katika Kaunti ya Mombasa, hatua ambayo amesema imechangia kupungua kwa visa vya uhalifu na utovu wa usalama vilivyokuwa vikishuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo. Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya usalama na wananchi.

Akizungumza katika eneo bunge la Jomvu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Miraj amesema ukanda wa Pwani kwa miaka mingi umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya matumizi na biashara ya mihadarati. Hata hivyo, amebainisha kuwa kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Usalama wa Ndani, vyombo vya usalama na serikali ya kaunti, hatua kubwa zimepigwa katika kudhibiti tatizo hilo. Amesema juhudi hizo zimewaokoa vijana wengi kutoka katika uraibu wa dawa za kulevya na kuwapa fursa ya kujijenga upya na kuboresha maisha yao.

Aidha, amewapongeza vijana pamoja na mashirika mbalimbali ya kijamii ambao wamejitolea kuwasaidia wenzao kuachana na matumizi ya dawa za kulevya kupitia ushauri nasaha, mafunzo ya stadi za maisha na programu za kuwawezesha kiuchumi. Akisema mchango wao umeleta matumaini kwa vijana wengi waliokuwa wamekata tamaa.

                                                 

Seneta huyo pia ametoa pongezi maalum kwa Mkurugenzi wa Shirika la Reachout, Taib Abdulrahman, kwa kujitolea kwake kupambana na tatizo la mihadarati na kuwawezesha vijana kupitia programu mbalimbali za urekebishaji na maendeleo. Akiitaka serikali kutambua na kuunga mkono juhudi zake pamoja na mashirika mengine yanayofanya kazi ya kuwaokoa vijana dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Miraj pia amempongeza Gavana wa Mombasa kwa juhudi zake za kupambana na matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya, akisema kampeni hizo zimeleta matokeo chanya. Amewataka vijana kuachana kabisa na matumizi ya mihadarati, wakisisitiza kuwa kufanya hivyo kutawapa nafasi ya kutimiza ndoto zao, kujijengea maisha bora na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Vilevile seneta Miraj ameitaka serikali kupeleka huduma za usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa moja kwa moja katika shule za ukanda wa Pwani ili kuwawezesha wanafunzi wengi kupata vyeti hivyo kwa urahisi. Akisema hatua hiyo itasaidia shule kusajili wanafunzi ipasavyo na kunufaika na mgao wa fedha unaotolewa na serikali kulingana na idadi halisi ya wanafunzi.

 

 


Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.