Serikali ya Kaunti ya Mombasa Yaonya Wanaojenga Bila Kuzingatia Sheria
Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeanzisha operesheni ya kukabiliana na miradi yote ya ujenzi inayoendelea bila kuzingatia masharti ya vibali na sheria za mipango ya mji, ikisema hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa umma na kuhakikisha maendeleo yanafanyika kwa utaratibu.
Kupitia taarifa iliyotolewa na wizara ya Ardhi, Mipango Miji, Makazi na Serikali Mitaani ikiongozwa na waziri Mohamed Husein Amadoh amesema kaunti hiyo imebaini ongezeko la miradi isiyofuata masharti ya vibali vya ujenzi pamoja na matakwa mengine ya kisheria, hali inayotishia usalama wa wananchi, mazingira na mpangilio wa miji.
Akisema licha ya kutoa notisi na maonyo kwa waendelezaji wa miradi na wamiliki wa majengo, baadhi yao wameendelea na shughuli za ujenzi kinyume cha sheria.
Amesema kutokana na hali hiyo, serikali ya kaunti imetangaza kuanza mara moja operesheni ya utekelezaji wa sheria katika maeneo yote ya kaunti ya Mombasa huku miradi itakayobainika kukiuka masharti ya vibali au sheria nyingine husika itachukuliwa hatua za kisheria.
Serikali ya Kaunti imewataka wajengaji wote kuhakikisha wanapata vibali vinavyohitajika kabla ya kuanza ujenzi na kuzingatia kikamilifu masharti yote yaliyowekwa na mamlaka husika.
Waziri wa ardhi, Mipango ya Miji, Makazi na Serikali Mitaani, Mohamed Hussein, amesema kaunti ya Mombasa itaendelea kusimamia maendeleo ya miji ili kuhakikisha Mombasa inakuwa na mazingira salama, yenye mpangilio mzuri na maendeleo endelevu kwa manufaa ya wakazi wote.
Comments
Post a Comment