Zaidi ya walimu wakuu 10,000 wa shule za sekondari kukongamana Mombasa katika warsha ya kila mwaka.

Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari nchini (KESSHA) umeanza Kongamano lake la 49 la Kitaifa la KCB/KESSHA katika Ukumbi wa Sheikh Zayed kaunti ya Mombasa, likiwakutanisha wakuu wa shule za sekondari kutoka maeneo mbalimbali nchini kujadili mustakabali wa elimu na utekelezaji wa Elimu ya Umilisi (CBE) huku zaidi ya walimu wakuu elfu kumi wakitarajiwa kuhudhuria.

Kongamano hilo la siku tano linaongozwa na kaulimbiu ya “Shule Imara na Uongozi wa Ushirikiano kwa Kuendeleza Elimu ya Umilisi.”


Akizungumza katika mkutano na wanahabari kabla ya kuanza kwa kongamano hilo, Mwenyekiti wa Kitaifa wa KESSHA, Willie Kuria, amesema kaulimbiu hiyo inaakisi dhamira ya chama hicho ya kuimarisha uongozi wa shule, kuendeleza ushirikiano kati ya wadau wa elimu, na kuhakikisha utekelezaji wenye mafanikio wa Elimu ya Umilisi nchini.


Kuria amesisitiza kuwa mageuzi ya sekta ya elimu yanahitaji taasisi imara, uongozi wenye maono, ushirikiano madhubuti na mafunzo endelevu kwa walimu na viongozi wa elimu.


Amesema wamependekeza hatua kali za kukabiliana na ongezeko la visa vya utovu wa nidhamu shuleni.


Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuwa wanafunzi watakaohusika katika vurugu za shule waondolewe kwenye usajili wa Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini Kenya (KNEC) na kuruhusiwa kujisajili upya baadaye.

Pia amependekeza kuwa wanafunzi wasiopenda kuendelea na masomo katika shule za bweni wahamishiwe shule za kutwa, huku ikisisitiza kuwa kubadilisha shule zote za bweni kuwa za kutwa hakutamaliza changamoto ya utovu wa nidhamu.


“Mapendekezo haya mapya yanalenga kukabiliana na utovu wa nidhamu shuleni. Kubadilisha shule za bweni kuwa za kutwa pekee hakuwezi kumaliza tatizo la vurugu mashuleni,” alisema Kuria.


Aidha ametoa wito wa kuongezwa kwa fedha za ruzuku kwa kila mwanafunzi, wakisema kiwango cha sasa cha shilingi 17,500 kwa kila mwanafunzi hakitoshelezi mahitaji ya utekelezaji wa Mtaala wa Umilisi (CBC).


Kuria alieleza kuwa kongamano la kila mwaka la KESSHA ni jukwaa muhimu linalowaleta pamoja wakuu wa shule za sekondari kutafakari masuala yanayoibuka katika sekta ya elimu, kubadilishana uzoefu na mbinu bora, kujifunza kutoka kwa wataalamu na watunga sera, pamoja na kutoa maoni ya kitaalamu kuhusu masuala yanayoathiri elimu na maendeleo ya taifa.


Washiriki wa kongamano hilo watajadili masuala mbalimbali ikiwemo uongozi katika mazingira ya elimu yanayobadilika, mabadiliko ya kidijitali shuleni, ujenzi wa taasisi imara za elimu na kuimarisha mageuzi yanayoendelea katika sekta ya elimu.


Kongamano hilo linatarajiwa kutoa jukwaa kwa viongozi wa elimu kubadilishana mawazo na kubuni mbinu bunifu zitakazosaidia kuboresha ubora na ufanisi wa elimu ya sekondari nchini.

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.