Vijana Mombasa Wanufaika na TukTuk Kutoka Kwa Mission Relief Africa Kukabiliana na Ukosefu wa Ajira
Vijana 25 kutoka familia zisizojiweza katika Kaunti ya Mombasa wamepokea TukTuk kupitia mpango wa kuwawezesha kiuchumi ulioanzishwa na Mission Relief Africa, hatua inayolenga kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa TukTuk hizo, Mwenyekiti wa Mission Relief Africa, Said Mabruk, alisema shirika hilo lilianzisha mpango huo ili kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazowakabili vijana wengi pamoja na ukosefu wa nafasi za ajira.
Amesema Mission Relief Africa, ambayo ni tawi la Mission Relief UK nchini Kenya, imejijengea sifa kupitia shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo usambazaji wa chakula kwa familia zenye mahitaji, ugawaji wa nyama wakati wa Eid, misaada ya dharura kwa maeneo yaliyoathiriwa na ukame, programu za kusaidia mayatima, uwezeshaji wa wanawake, uchimbaji wa visima vya maji na miradi ya maendeleo ya jamii.
Said ameeleza kuwa mwaka huu pekee shirika hilo limefikia familia zaidi ya 10,000 kupitia mpango wa ugawaji wa nyama ya Eid, huku likiendelea kutafuta suluhu za muda mrefu za kuwawezesha wananchi kujitegemea.
"Changamoto inayowakabili vijana wengi leo si ukosefu wa ari ya kufanya kazi bali ni ukosefu wa fursa na rasilimali. Tumeshuhudia vijana wengi wakihitimu masomo au mafunzo lakini wakikosa ajira kwa miaka mingi. Miradi kama huu inalenga kuwapa fursa za kujipatia kipato na kusaidia familia zao," alisema.
Ameongeza kuwa TukTuk hizo zimetolewa kupitia mfumo wa mfuko wa mzunguko (revolving fund), utakaowezesha wanufaika zaidi kufaidika na mpango huo siku zijazo.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Mohammed Noor, alipongeza mpango huo akisema sekta ya usafiri wa TukTuk ni miongoni mwa sekta zinazoajiri watu wengi zaidi katika kaunti hiyo.
"Sekta ya TukTuk ndiyo mwajiri wa pili kwa ukubwa Mombasa baada ya Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA). Maelfu ya familia hutegemea sekta hii kwa maisha yao. Miradi kama hii inaongeza nafasi za ajira kwa vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi," alisema.
Aidha, Said Mabruk ametambua mchango wa Ali Nuno kwa ushirikiano wake wa karibu na Mission Relief Africa, akisema amekuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha miradi ya shirika hilo inawafikia walengwa na kuchangia kuimarisha usalama wa jamii.
Miongoni mwa wanufaika hao ni Ahmed Mbarak, mwenye umri wa miaka 27 kutoka Kisauni, ambaye amesema amekuwa akitegemea kazi za vibarua kwa muda mrefu bila uhakika wa kipato cha kudumu.
"Kwa muda mrefu nimekuwa nikifanya kazi za hapa na pale, lakini hazikuwa na uhakika. Siku nyingine kulikuwa na kazi na nyingine hakukuwa na kazi. Nina matumaini kuwa TukTuk hii itanisaidia kupata kipato cha kudumu na kuitunza familia yangu vizuri zaidi," amesema Ahmed.
Kwa upande wake, Mustafa Bakari kutoka Nyali alisema mpango huo umefungua ukurasa mpya maishani mwake baada ya miaka ya kutokuwa na uhakika wa ajira.
"Nilikata tamaa mara kadhaa kwa sababu sikuweza kupata kazi ya kudumu. Sasa nina nafasi ya kujiajiri na kuwahudumia watoto wangu," amesema.
Shirika hilo pia lilitoa shukrani kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, wafadhili wake pamoja na Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano wao katika kufanikisha miradi ya maendeleo inayolenga kuwawezesha vijana na kupunguza changamoto za kijamii zinazotokana na ukosefu wa ajira.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na maafisa wa serikali ya kitaifa na kaunti, viongozi wa usalama, viongozi wa jamii pamoja na washirika wa maendeleo.
Comments
Post a Comment