Waziri Amadoh Awahimiza Wakazi wa Mwakirunge Kuunga Mkono Miradi ya Maendeleo.
Huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ukizidi kukaribia na siasa zikipamba moto katika Kaunti ya Mombasa, Waziri wa Ardhi, Makao na Ustawi wa Jiji la Mombasa, Mohammed Hussein Amadoh, amewatahadharisha wakazi wa kaunti hiyo dhidi ya kuhadaiwa kisiasa na kushawishiwa kupinga miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao na wakazi wa eneo la Guu Ng'ombe-Mwakirunge, katika Eneo Bunge la Kisauni, Amadoh amesema ni muhimu kwa wananchi kuwa makini na kauli zinazotolewa na viongozi wa kisiasa, hasa kuhusu masuala ya maendeleo na umiliki wa ardhi.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuunga mkono miradi inayolenga kuboresha maisha yao na kuhakikisha kuwa masuala ya kisiasa hayatatumiwa kuzuia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo.
Kauli zake zimeungwa mkono na Mwakilishi wa Wadi ya Mwakirunge, Mwinyi Mtoto, ambaye ameitaka Serikali ya Kaunti ya Mombasa kuimarisha ushirikiano na wakazi wa eneo hilo ili kufanikisha maendeleo sawia na kuharakisha zoezi la ugavi wa hatimiliki za ardhi.
Kwa upande wao, wakazi wakiongozwa na John Jefwa na Purity Kadzo waliitaka serikali kuanzisha mchakato wa utoaji wa hatimiliki za ardhi kwa wakazi wa eneo hilo, wakisema hatua hiyo itawawezesha kunufaika kikamilifu na miradi ya maendeleo inayopangwa kutekelezwa na serikali.
Wakazi hao wameeleza kuwa umiliki rasmi wa ardhi kupitia hatimiliki utachangia kuboresha maisha yao kiuchumi na kuimarisha usalama wa makazi yao.




Comments
Post a Comment