Wafanyabiashara wadogo 3000 kufaidika na mafunzo na fedha kutoka kwa Benki ya Absa na Google Hustle Academy.

                                                        


Benki ya Absa Kenya PLC kwa ushirikiano na Google Hustle Academy wametangaza ushirikiano wa kimkakati unaolenga kutoa mafunzo ya biashara na msaada wa kifedha kwa wafanyabiashara wadogo (SMEs) 3,000 nchini katika kipindi cha miezi 12 ijayo.

Mpango huo unalenga kuwafikia na kuwawezesha wafanyabiashara kwa kuwapa ujuzi wa kidijitali, maarifa ya kifedha, mikakati ya kukuza biashara pamoja na mwongozo wa kurasimisha na kupanua shughuli zao kwa njia endelevu.Kufikia sasa, programu hiyo imefaidi makundi matatu ya mafunzo yaliyohudhuriwa na zaidi ya wafanyabiashara 600.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Absa Bank Kenya, Renato D’Souza, amesema benki hiyo imejitolea kuwawezesha wafanyabiashara kwa kuwapatia zana na rasilimali wanazohitaji kufanikiwa.

“Tunafurahia kushirikiana na Google kupeleka Hustle Academy kwa wajasiriamali wengi zaidi nchini Kenya. Kwa kuunganisha utaalamu wa kidijitali wa Google na suluhisho zetu za kifedha, tuna imani kuwa tutasaidia biashara ndogo na za kati kurasimisha na kukuza shughuli zao,” amesema.

Kupitia ushirikiano huo, Absa Bank Kenya itawapa washiriki ushauri wa kifedha, huduma za ushauri wa biashara, pamoja na fursa za kupata bidhaa maalum za benki kwa biashara ndogo na za kati, ikiwemo mikopo, zana za usimamizi wa mtiririko wa fedha na fursa za masoko.

                                       

Kwa upande wake, Kristy Grant wa Google Hustle Academy amesema mustakabali wa uchumi wa kidijitali barani Afrika uko mikononi mwa wajasiriamali na watu binafsi.

“Tunaamini kuwa kwa kuwapa watu mafunzo ya matumizi ya zana za kisasa zinazotumia Akili mnemba AI, tunajenga msingi wa ukuaji wa muda mrefu na kuwaunganisha moja kwa moja na bidhaa za kiwango cha kimataifa za Google,” amesema.

Google Hustle Academy ni kambi ya mafunzo ya siku moja inayofanyika mtandaoni bila malipo, iliyobuniwa kusaidia biashara ndogo kustawi katika uchumi wa kidijitali. Mpango huo unalenga kuwafundisha washiriki matumizi ya zana na mbinu za kisasa zinazotegemea Akili mnemba (AI), huku ikiwaunganisha moja kwa moja na bidhaa na huduma za Google ili kusaidia ukuaji wa biashara zao.

Mafunzo hayo yanajumuisha warsha za vitendo, vipindi vya ushauri kutoka kwa wataalamu pamoja na fursa za kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wenzao, ili kuhakikisha washiriki wanapata maarifa yanayoweza kutumika moja kwa moja katika biashara zao.


Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.