Kenya Yasisitiza Ushirikiano wa Kimataifa katika Kuhifadhi Bahari.

 


Serikali ya Kenya imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kulinda mifumo ya ikolojia ya bahari na kuimarisha uchumi samawati wakati viongozi na wadau kutoka mataifa mbalimbali wakikutana katika Our Ocean Conference linalofanyika kaunti ya Mombasa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa kongamano hilo katika Hoteli ya PrideInn,naibu wa rais Kithure Kindiki amesema uhusiano wa Afrika na bahari ni wa kihistoria, wa kina na wa kudumu, akibainisha kuwa pwani, bandari na mifumo ya ikolojia ya bahari imekuwa msingi wa ustawi wa jamii nyingi kwa karne nyingi kupitia biashara, utamaduni na uchumi.

                                           

Amesema uchumi wa bahari duniani kwa sasa unakadiriwa kuwa na thamani ya takribani dola trilioni 3.3 za Marekani kwa mwaka, sawa na asilimia 2.5 ya pato la taifa la dunia, huku ukitarajiwa kufikia dola trilioni 5.5 ifikapo mwaka 2030 kupitia sekta kama usafirishaji wa majini, uvuvi, utalii wa pwani, nishati ya baharini na teknolojia ya viumbe wa majini.

Amesisitiza kuwa uchumi samawati haupaswi kuangazia tu uchimbaji wa rasilimali za bahari, bali pia usimamizi endelevu ili kuhakikisha mifumo ya ikolojia ya bahari inalindwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Taifa la Kenya limethibitisha upya kujitolea kwake kutekeleza makubaliano ya kimataifa ya mazingira, yakiwemo Makubaliano ya Paris, Mfumo wa Kimataifa wa Bayoanuai wa Kunming-Montreal na lengo la kulinda asilimia 30 ya maeneo ya baharini na pwani ifikapo mwaka 2030.

                                                

Aidha, Kenya imeahidi kuharakisha utekelezaji wa Makubaliano ya BBNJ barani Afrika na kuimarisha juhudi za kukabiliana na uchafuzi wa plastiki kupitia mikataba ya kimataifa yenye nguvu za kisheria.

Kiongozi huyo pia ameeleza kuwa Kenya inaendelea kupanua maeneo ya hifadhi za bahari, kurejesha mikoko na nyasi za bahari, kuunda ajira za sekta ya baharini, kujenga bandari rafiki kwa mazingira na kuwekeza katika miradi ya kaboni pamoja na nishati mbadala inayotokana na bahari.

Amesisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kukabiliana na changamoto za bahari peke yake, akitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano katika nyanja za ufadhili, teknolojia, ubunifu na ujenzi wa uwezo.

                                                 

Kindiki amewataka wajumbe kubadili ahadi kuwa vitendo na kufanya kongamano hilo kuwa hatua muhimu katika juhudi za kimataifa za kulinda bahari.

Kongamano hilo limefunguliwa rasmi kwa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kuhakikisha bahari inakuwa salama, safi na zenye ustahimilivu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kongamano hilo linafanyika chini ya kaulimbiu "Bahari Yetu, Urithi Wetu, Mustakabali Wetu", wakati ambapo dunia inakabiliwa na changamoto zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na shughuli za kibinadamu zinazoweka shinikizo kubwa kwa bahari.

                                                           


Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.