Wasichana Wawili wa kidato Cha tatu Watoweka Mombasa, Familia Zikililia usalama wao.
Familia za wasichana wawili waliotoweka mjini Mombasa zimeomba msaada wa umma katika juhudi za kuwapata, huku hofu ikizidi kuibuka kuhusu usalama wao.
Wasichana hao, Vanessa mwenye umri wa miaka 16 na Teriana mwenye miaka 17, ni wanafunzi wa Kidato cha Tatu ambao hawajaonekana tangu Jumanne ya tarehe 25 agosti baada ya kutumwa dukani kununua bidhaa.
Kwa mujibu wa familia, wasichana hao waliondoka nyumbani majira ya saa 8 mchana kwenda kununua maziwa na mkate, lakini hawakurejea nyumbani.
Joyce Kimani, ambaye ni mama wa mmoja wa wasichana hao, amesema yeye ndiye aliyewatuma dukani kununua maziwa na baada ya hapo hawajaonekana tena.
«“Niliwatuma kununua maziwa na mkate. Tangu wakati huo sijawaona tena,” alisema Kemani.»
Amesema familia imekuwa ikipitia wakati mgumu tangu watoto hao walipotoweka, huku baadhi ya wanafamilia wakishindwa kula na kulala kutokana na wasiwasi.
Kimani amewaomba watu ambao huenda wamewaona wasichana hao kutoa taarifa katika kituo cha polisi kilicho karibu badala ya kuwadhuru.
«“Tafadhali, ikiwa kuna mtu amewaona, asiwaondoe. Awapeleke tu katika kituo cha polisi. Tunataka kuwaona watoto wetu wakirejea shuleni kwa sababu tuko kwenye maumivu,” amesema.»
Tabitha Mbuto ambaye pia ni mmoja wa wanafamilia, amesema wasichana hao waliondoka nyumbani wakiwa na furaha na hakukuwa na dalili zozote za kuwa walikuwa na matatizo nyumbani.
Amesema familia inaomba msaada wa kila mtu mwenye uwezo wa kuwasaidia kuwapata watoto hao ili warejee nyumbani na kuendelea na masomo yao.
«“Tunamuomba Mungu atupe ujasiri ili tuweze kuwapata watoto wetu. Tunapowafikiria watoto wetu, wanapaswa kuwa shuleni sasa. Wako Kidato cha Tatu na huu ni wakati muhimu wa kujiandaa kwa mitihani yao,” amesema.»
Familia hizo zimesema tayari zimetoa taarifa kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na zinaendelea kushirikiana na maafisa wa usalama katika juhudi za kuwatafuta wasichana hao.
Kwa mujibu wa familia, juhudi hizo pia zinahusisha kufuatilia simu iliyokuwa ikitumiwa na mmoja wa wasichana hao ili kubaini eneo lake la mwisho.
Salma Ahmed mkurugenzi WA shirika la SHE RISES amesema visa vya wasichana na vijana kutoweka vinaonekana kujirudia katika kaunti ya Mombasa.
Amesema wasichana hao bado ni watoto na ametoa wito kwa yeyote anayefahamu walipo kuwafikisha mara moja katika kituo cha polisi kilicho karibu.
«“Hawa wawili bado ni watoto. Yeyote atakayekutana na Teriana au Vanessa, tafadhali awapeleke katika kituo cha polisi kilicho karibu ili wazazi wao waweze kuungana nao,” amesema Salma.
Salma pia amezitaka mamlaka kuharakisha uchunguzi na kutumia kila njia inayowezekana kuhakikisha wasichana hao wanapatikana wakiwa salama.
Familia zimesema kutoweka kwa wasichana hao kumesababisha maumivu makubwa kwa wazazi, ndugu na jamaa zao.
Wazazi hao sasa wanatoa wito kwa umma, maafisa wa usalama na mtu yeyote mwenye taarifa kuhusu Vanessa na Teriana kujitokeza na kusaidia katika juhudi za kuwapata.
Familia hizo pia zimeeleza imani yao kwa DCI katika kuendeleza uchunguzi, huku zikimuomba Mungu awezeshe wasichana hao kupatikana wakiwa salama na kurejea nyumbani.
Comments
Post a Comment