Wabunge Wasukuma Mageuzi katika Kilimo na Uchumi Samawati Katika Maonyesho ya Kilimo Mombasa.




Wabunge waliohudhuria maonyesho ya kilimo  kwenye uwanja wa Mkomani Showground wamesema bunge linaendelea kusukuma sera zinazolenga kupunguza gharama za pembejeo za kilimo, kuboresha masoko na kulinda maslahi ya wakulima na wavuvi.

Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo ya Bunge la Kitaifa, Brighton Yegon, amesema wakulima wanapaswa kulindwa dhidi ya gharama kubwa za uzalishaji pamoja na unyonyaji wa kibiashara

Yegon akiweka wazi kuwa ukame na hali ya hewa baridi ni miongoni mwa sababu zinazochangia kupungua kwa uzalishaji wa maziwa nchini.
                  
                                   

Yegon amesema sehemu kubwa ya maziwa nchini huzalishwa na wakulima wadogo, ambao huathirika zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema wakati wa ukame na hali mbaya ya hewa, wakulima hushindwa kupata chakula cha kutosha kwa mifugo, hali inayosababisha ng’ombe kudhoofika na hatimaye kupunguza kiwango cha maziwa wanachozalisha.

Kwa mujibu wa Yegon, serikali imepanga kupunguza bei ya mbolea ili kuwawezesha wakulima wadogo kupata pembejeo kwa bei nafuu, kuongeza uzalishaji wa mazao pamoja na kupanda nyasi na mimea ya kutosha kwa ajili ya kulisha mifugo.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko amesema lengo la maonyesho ya kilimo ni kuwawezesha wakulima na wananchi kujifunza mbinu za kisasa za kilimo, kupata ujuzi mpya na kuboresha shughuli zao za kilimo na kupata fursa za kujiendeleza katika sekta ya uchumi samawati.

Amesema kuna taasisi mbalimbali zinazotoa misaada ya kifedha na mafunzo kwa wakulima ili kuwawezesha kuendeleza shughuli zao, kuongeza thamani ya bidhaa na kupata masoko ya ndani na kimataifa.

Mboko amewataka wananchi wanaotembelea maonyesho hayo kutumia fursa hiyo kujifunza kutoka kwa waonyeshaji mbalimbali waliopo katika maonyesho hayo.

                                  

Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa samawati ili kujiajiri, kuongeza kipato na kuboresha maisha yao, akisema sekta hiyo ina fursa nyingi ambazo bado hazijatumika kikamilifu.

Akiweka wazi kuwa ukanda wa Pwani bado haijanufaika kikamilifu na utajiri wa bahari, akitoa wito wa matumizi ya teknolojia bunifu na kuongeza thamani ya bidhaa za baharini ili jamii za maeneo ya Pwani zinufaike zaidi.

Kwa upande wake, Seneta Mteule wa Vijana, Hezena Lemelatian, amewataka vijana kujenga mahusiano mazuri na watu wanaoweza kuwasaidia kukua na kujiendeleza kimaisha.

Hezena amesema maonyesho ya kilimo yanatoa fursa kubwa kwa vijana kukutana na wataalamu, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wenye ujuzi katika sekta ya kilimo na uchumi wa samawati.

Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo kujenga mitandao, kubadilishana mawazo na kupata maarifa ambayo yanaweza kuwasaidia kuanzisha au kukuza shughuli zao za kiuchumi.

                         
Amewataka pia vijana kutumia maonyesho hayo kukutana na wakurugenzi na viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali na kuwawasilishia mapendekezo pamoja na mawazo yao kuhusu miradi ya kilimo na uchumi wa samawati.

Hezena amesema hatua hiyo inaweza kuwasaidia vijana kupata usaidizi, fursa za ajira, mafunzo na uwezeshaji wa miradi yao.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Utangazaji na Maktaba, Julius Kipletting Rutto, amesema Bunge linatumia majukwaa yake ya mawasiliano kuwawezesha Wakenya kupata taarifa kuhusu sheria zinazopitishwa pamoja na shughuli za uangalizi wa serikali.

                                                

Wabunge hao wamewahimiza Wakenya kutumia maonyesho hayo si kwa burudani pekee, bali pia kujifunza kuhusu teknolojia za kisasa za kilimo pamoja na kufahamu nafasi ya Bunge katika utungaji wa sheria, uwakilishi wa wananchi na uangalizi wa shughuli za serikali.


Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.