Ujenzi wa kiwanda Cha gesi Dongo Kundu wafikia asilimia 85.
Ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuhifadhi gesi ya kupikia kinachojengwa na kampuni ya Taifa Gas kutoka Tanzania katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Dongo Kundu umefikia asilimia 85.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 15, unajumuisha matangi 12 ya kuhifadhi gesi, ambapo kila tanki lina uwezo wa kuhifadhi tani 2,500,hivyo kutoa uwezo wa jumla wa kuhifadhi tani 30,000.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo,katibu katika idara ya uchukuzi Mohamed Daghar amesema kampuni ya Taifa Gas ni mwekezaji wa kwanza kuanzisha kituo kikubwa cha aina hiyo katika eneo hilo.
Daghar amesema kituo hicho kitakuwa kikubwa zaidi nchini Kenya na katika ukanda wa Afrika, huku kikitarajiwa kuchangia kupunguza bei ya gesi kwa kuwezesha kununuliwa kwa wingi, kuhifadhiwa nchini na kusambazwa katika soko la Kenya pamoja na nchi jirani.
Akiweka wazi kuwa gharama ya nishati nchini imekuwa juu, lakini uwekezaji kama huo utasaidia kupunguza bei kutokana na uwezo wa kununua gesi kwa wingi na kupata faida ya uzalishaji na usambazaji wa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA), Capt William Ruto, amesema mradi huo tayari umewezesha kupatikana Kwa nafasi za ajira zaidi ya 500, huku nafasi zaidi zikitarajiwa baada ya kukamilika na kuanza kwa shughuli rasmi.
Ruto amesema wenyeji watanufaika pia kupitia mafunzo yatakayowawezesha kupata ujuzi wa kushughulikia gesi kwa usalama na kufanya kazi katika sekta hiyo.
Amesema ukubwa wa kituo hicho utaiwezesha Kenya kunufaika na uchumi wa kiwango,jambo litakalosaidia kupunguza gharama ya gesi ya kupikia kwa watumiaji.
Aidha, amesema kituo hicho kitaunganishwa na miundombinu ya kisasa ya mafuta katika Bandari ya Mombasa, ambayo itawezesha bandari kushughulikia meli kubwa za kubeba gesi na hivyo kuimarisha nafasi ya Mombasa kama kitovu cha nishati katika ukanda huu.
Meneja wa Mradi huo Mohamad Rod, amesema ujenzi umefikia asilimia 85, huku sehemu kubwa ya kazi za mitambo ikiwa imekamilika.
Rod amesema vifaa vyote muhimu vimewasili na mchakato wa ununuzi wa vifaa umekamilika, huku kampuni ikielekeza nguvu katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza shughuli.
Amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika katika mwishoni mwa mwaka huu.
Comments
Post a Comment