Serikali Yaongeza Juhudi za Kuimarisha Usalama wa Chakula na Kilimo Pwani.

                                   


Serikali imezindua mkakati wa kuimarisha uzalishaji wa kilimo, uchakataji, biashara na usafirishaji katika eneo la Pwani kupitia mpango wa “From Farm to Port” (Shamba hadi Bandarini).

Akizungumza Alhamisi, Septemba 3, 2026, wakati wa ufunguzi rasmi wa Mombasa International Show katika uwanja wa Mkomani Showgrounds, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Seneta Mutahi Kagwe, amesema mpango huo unalenga kuunganisha uzalishaji wa mazao katika kaunti za Pwani na masoko ya ndani na kimataifa.

Kwa mujibu wa Kagwe, kaunti za Kwale, Kilifi, Taita Taveta na Tana River zitazingatia uzalishaji wa kilimo na kuongeza thamani ya bidhaa, huku Mombasa na Lamu zikitumika kama vituo muhimu vya usafirishaji na ugavi vinavyounganisha eneo hilo na Kenya, Afrika Mashariki na masoko ya dunia.

Kagwe amesema kaunti za Pwani bado hazijatumia kikamilifu uwezo wao wa kilimo na ufugaji, akitaja korosho, nazi, mihogo, pamba, maziwa na nyama miongoni mwa bidhaa zinazoweza kuongeza uzalishaji mara tatu au hata mara nne.

                                  

Akisema Serikali na washirika wake wamekuwa wakitekeleza mipango ya kufufua uchumi wa Pwani, huku uwekezaji mpya ukitarajiwa kuongeza ajira na fursa za biashara.

Akisema mwekezaji kutoka Uswizi anawekeza katika kituo cha thamani ya mamilioni ya fedha katika Dongo Kundu Special Economic Zone, kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mpya za chai.

Pia, mpango wa kibiashara wa ardhi ya ekari milioni moja huko Galana Kulalu unaendelea, huku kampuni binafsi zikiwa tayari zimewekeza takribani bilioni 9 katika ujenzi wa miundombinu na uzalishaji wa mahindi, vitunguu, njegere na karoti.

Serikali pia imeimarisha juhudi za kufufua sekta ya korosho kupitia usambazaji wa miche yenye ruzuku kwa lengo la kuongeza mashamba, uzalishaji, uchakataji na mapato ya wakulima.

                                       

Kagwe amesema mwaka 2025, eneo linalolimwa korosho liliongezeka kwa zaidi ya hekta 1,900, huku uzalishaji ukiongezeka kwa tani 588 hadi kufikia tani 8,397, zenye thamani ya Sh546 milioni.

Kwa upande wa nazi, alisema sekta hiyo inatoa ajira na riziki kwa zaidi ya familia 100,000 za wakulima katika Pwani.

Serikali inalenga kuongeza thamani ya nazi kupitia bidhaa kama mafuta ya nazi, maji ya nazi, unga wa nazi, krimu na maziwa ya nazi. Mwaka 2025, zaidi ya tani 100,000 za nazi zilitolewa zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh10.8 bilioni.

Kagwe amesema eneo linalolimwa pamba limeongezeka kutoka hekta 8,579 mwaka 2022 hadi hekta 18,852 mwaka 2026.

Uzalishaji umeongezeka kutoka marobota 6,779 ya kilo 185 mwaka 2022 hadi marobota 15,892 mwaka 2026, huku wakulima wakipata mapato ya takribani Sh697 milioni mwaka huo.

Serikali inalenga kuongeza uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa pamba ili kupunguza uagizaji wa vitambaa kwa asilimia 50 na kuongeza mauzo ya nje hadi Sh150 bilioni kufikia mwaka 2027.

                                     

Serikali imetangaza kupunguza gharama ya mbolea yenye ruzuku kutoka Sh2,500 hadi Sh2,000 kwa mfuko wa kilo 50, pamoja na kutoa ruzuku kwa mbegu za mahindi.

Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikikadiria kuwa uzalishaji wa mahindi wa mwaka 2026 unaweza kusababisha upungufu wa kitaifa wa magunia 42,580,768 ya kilo 90.

Serikali pia imesema kupitia NCPB itawezesha uagizaji wa mahindi kutoka nje ili kuhakikisha usalama wa chakula na kuwalinda walaji dhidi ya ongezeko la bei linaloweza kusababishwa na upungufu wa uzalishaji.

Licha ya hatua zilizochukuliwa, Waziri Kagwe amesema wakulima wa Pwani bado wanakabiliwa na changamoto kama mvua zisizotabirika, gharama kubwa za pembejeo, kupungua kwa rutuba ya udongo na wadudu waharibifu.

Changamoto nyingine ni miundombinu duni, ukosefu wa mikopo ya kutosha na kupungua kwa ukubwa wa mashamba.

                                    

Serikali, kwa kushirikiana na kaunti, inalenga kukabiliana na changamoto hizo kupitia umwagiliaji, kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, udhibiti wa magonjwa na wadudu pamoja na kuongeza upatikanaji wa pembejeo.

Mipango mingine ni pamoja na kuendeleza minyororo ya thamani ya nazi, korosho, maembe, pamba na sukari, kuimarisha kilimo cha mpunga na umwagiliaji Tana River na Kwale, biashara ya mifugo Taita Taveta, Kwale na Lamu, pamoja na programu za uvuvi na ufugaji wa samaki.

Kagwe akisema Serikali pia itaendelea kuunga mkono vituo vya uchakataji wa mazao na matumizi ya County Aggregation and Industrial Parks ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kufikishwa sokoni.

Mombasa International Show ya mwaka huu inaendeshwa chini ya kaulimbiu “Promoting Climate Smart Agriculture and Trade Initiatives for Sustainable Economic Growth”, inayolenga kukuza kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi na biashara kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi. 

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.