Serikali yaharakisha utekelezaji wa mradi wa bilioni 75 WA Dongo Kundu,Yalenga ukamilike 2028.
Serikali imeongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa Dongo Kundu Special Economic Zone (SEZ),huku wawekezaji 94 wakiwa wamewasilisha maombi ya kuwekeza katika eneo hilo.
Katibu katika Wizara ya Uchukuzi, Mohamed Daghar amesema zaidi ya taasisi 10 za serikali zimefanya ukaguzi wa mradi huo wa kimkakati ili kutathmini maendeleo yake na kushughulikia changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji wake.
Amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 75 unahusisha ujenzi wa gati, barabara, miundombinu ya umeme na maji.
Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) inajenga gati la kwanza kati ya saba, lenye urefu wa mita 300, ambalo litawezesha meli kubwa ikiwemo Panamax kutia nanga katika eneo hilo.
Kwa sasa, ujenzi wa gati hilo umefikia asilimia 16, huku KPA ikisema kazi iko mbele ya ratiba kwa takribani asilimia mbili.Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2028,ila serikali inalenga kuharakisha utekelezaji wake ukamilike mapema.
Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 4.6, njia panda ya kilomita 2.8 huku KETRACO inatarajiwa kujenga njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 51 kutoka Mariakani, ikiwa na uwezo wa 220kV na mfumo wa double circuit.
Serikali pia inatekeleza mradi wa maji kutoka Tiwi, Kaunti ya Kwale, pamoja na kuunganisha maji kutoka bwawa la Mwache.
Dongo Kundu yote inakalia takribani ekari 3,000, huku eneo la Mombasa Special Economic Zone likichukua takribani ekari 1,700.
Baadhi ya wawekezaji tayari wameanza shughuli zao, akiwemo Taifa Gas, ambayo inakaribia kukamilisha ujenzi wa kiwanda chake cha gesi.
Wawekezaji wengine wameonyesha nia ya kuanzisha kiwanda cha chuma, kiwanda cha vioo, kituo cha kuhifadhi bidhaa kwa baridi pamoja na shughuli nyingine za kibiashara na kiviwanda.
Mohamed amesema serikali pia ina mfumo wa uwekezaji na Afreximbank unaolenga kuvutia takribani dola bilioni moja za uwekezaji na kuchochea uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA Capt William Ruto, amesema mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa gati yuko mbele ya ratiba na serikali inalenga kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati au kabla ya muda uliowekwa.
Ruto amesema kati ya wawekezaji 94 waliowasilisha maombi, takribani wanne tayari wamechukua maeneo, huku wengine wakisubiri kukamilika kwa gati ili kuanza uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa.
Serikali inatarajia Dongo Kundu SEZ kuwa kitovu cha viwanda, biashara na usafirishaji, huku bidhaa zitakazozalishwa katika eneo hilo zikisafirishwa kupitia Bandari ya Mombasa kwenda masoko ya ndani, Afrika Mashariki na kimataifa.
Mradi huo unatarajiwa pia kuongeza shughuli za Bandari ya Mombasa, kuvutia uwekezaji wa kigeni na kutoa maelfu ya ajira kwa Wakenya katika sekta mbalimbali.
Comments
Post a Comment