ODM Mombasa Yawaonya viongozi wa UDA kukoma Kuwashambulia Viongozi Wao.

     

Viongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kaunti ya Mombasa wamewataka wenzao wa United Democratic Alliance (UDA) kukoma kuwashambulia  na kuwakosoa viongozi wa ODM, wakisema vyama hivyo ni washirika katika serikali jumuishi na Wala si maadui.

Wakizungumza katika kaunti ya Mombasa,wakiongozwa na Mwenyekiti wao katika kaunti hiyo Mohamed Hamid Khamis amesema viongozi na wanachama wa ODM katika kaunti hiyo wamekuwa wakihamasisha wananchi kumuunga mkono Rais William Ruto na kueleza ajenda zake za maendeleo anapolenga kuwania muhula wa pili wa urais.
   

Khamis amehoji sababu ya baadhi ya viongozi wa UDA kulenga kuwashambulia viongozi wa ODM badala ya kushirikiana katika kuwasilisha ajenda ya serikali jumuishi.

“Tunawauliza wenzetu wa UDA, sisi ni maadui wenu ama ni washirika wenu?” Khamis ameuliza.

Amesema chama Cha  ODM Mombasa kitaendelea kuwahamasisha wanachama wake kumuunga mkono Rais Ruto, akisisitiza kuwa chama hicho kina miundo imara ya mashinani Mombasa na Pwani Kwa jumla.

Khamis amesema ODM itahakikisha kura za wanachama wake na wafuasi Mombasa zinaelekezwa kwa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Amesema ujuzi nantajriba alionao kama kiongozi ni wa kuwashawishi wananchi kujitokeza na kupiga kura kwa wingi, na wala si kupigisha kura watu waliokufa kama baadhi ya viongozi wanavyodai.

Kauli hizo zinajiri wakati kukiwa na tofauti za kisiasa kati ya wafuasi wa ODM na UDA Mombasa kuhusu uchaguzi wa 2027, hususan suala la vyama hivyo kuwania nyadhifa za kaunti kwa kujitegemea.

Katibu wa ODM kaunti ya Mombasa Joffrey Busaka ameunga mkono kauli hizo akisema chama hicho kinaheshimu ushirikiano wa serikali jumuishi lakini hakitakubali viongozi wake kushambuliwa.
      

Busaka amesema jukumu la ODM katika ushirikiano huo ni kushiriki katika uhamasishaji wa kura za kumuunga mkono Rais Ruto, akipuuzia hofu kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mpangilio wa kugawana maeneo ya kisiasa(zoning) akiwataka wanaopinga msimamo wa ODM kuwa tayari kwa uchaguzi.

“Bring it on. Tuko tayari. Kila mtu asimame na tutakabiliana naye,” Busaka amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ODM Women's League Mombasa, Milka Moraa Ngare, ametoa wito wa kuheshimiana kati ya viongozi wa ODM na UDA, akisema vyama hivyo vinapaswa kuelekeza nguvu katika kutafuta kura za kumuunga mkono Rais Ruto badala ya kushambuliana.
    

Ngare amesema wanachama wa ODM wamekuwa wakijizuia kwa muda mrefu kwa sababu wanatambua UDA kama mshirika wao katika serikali jumuishi.

Kauli za viongozi hao zinajiri siku chache baada ya Rais William Ruto kusisitiza kuwa ODM na UDA ni washirika na wala si washindani katika mfumo wa serikali jumuishi.

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.