Mzozo wa Umiliki wa Ardhi ya Shilingi Bilioni 1.5 Wazuka Samburu kaunti ya Kwale.
Mgogoro wa umiliki wa shamba lenye ukubwa wa ekari 3,100 na thamani ya Shilingi bilioni 1.5 umezuka eneo la Samburu, Kaunti ya Kwale, huku aliyekuwa mwakilishi wadi Saidi Mung’aro Nzuga na Rev. Fredrick Kanato Ndaikwa wakidai kuwa wao ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo.
Nzuga amesema yeye pamoja na Kanato walinunua shamba hilo kutoka kwa familia ya Mwachizi mwaka 2018, wakidai kuwa walifuata taratibu zote za kisheria na kufikia makubaliano rasmi na familia hiyo.
Amesema wana nyaraka na barua mbalimbali zinazothibitisha kuwa walipata ardhi hiyo kihalali. Aidha, amefichua kuwa hati ya umiliki wa ardhi hiyo ilitolewa mwezi Aprili mwaka huu, baada kuhangaika kwa muda wa miaka Saba.
Hata hivyo, Nzuga anadai kuwa mhandisi Lung’azi Chai, ambaye analenga kuwania ugavana wa Kaunti ya Kwale, amejitokeza na kudai kuwa alinunua shamba hilo mwaka 2024 na kwamba ndiye mmiliki halali.
Nzuga anadai kuwa Lung’azi ameweka watu katika eneo hilo kwa ajili ya kulinda shamba hilo, huku akiwatishia watu wanaojaribu kuingia katika eneo hilo.
Aliyekuwa mwakilishi wadi huyo ameitaka Serikali kuingilia kati mzozo huo na kuhakikisha haki inatendeka. Anadai kuwa baadhi ya maafisa wa Serikali, akiwemo Naibu Kamishna wa Kaunti wa eneo hilo, wanashirikiana na upande wa Lung’azi katika kile anachodai ni jaribio la kuwanyang’anya ardhi yao.
Nzuga ameipa Serikali makataa ya wiki moja kushughulikia suala hilo, akisema iwapo hatua haitachukuliwa, wataingia katika shamba hilo. Amesema pia yuko tayari kufikisha suala hilo mahakamani ili kuthibitisha uhalali wa umiliki wao.
Kwa upande wake, Rev. Fredrick Kanato Ndaikwa amesema wamedhulumiwa katika suala hilo licha ya kuwa na nyaraka anazodai ni halali za umiliki wa ardhi hiyo.
Kanato amesema yeye na Nzuga wametumia zaidi ya Shilingi milioni 6 katika harakati za kupata hati ya umiliki wa shamba hilo.
Aidha, amedai kuwa walitumia takriban Shilingi milioni 1.6 katika ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti katika mchakato huo. Pia amedai kuwa baadhi ya viongozi waliwahi kuwahitaji walipe fedha ili kuwasaidia kupata hati miliki.
Kanato ameitaka Serikali Kuu kuingilia kati suala hilo na kumwondoa Naibu Kamishna wa Kaunti wa eneo hilo, ambaye anamtuhumu kwa kushindwa kuwasaidia wananchi. Pia amemtaka Rais William Ruto kuchukua hatua dhidi ya afisa huyo.
Kanato amedai pia kuwa watu waliowekwa katika shamba hilo walifika wakiwa na silaha na kuanza kuweka ulinzi. Amewataka kuondoka katika eneo hilo mara moja ili kuepusha machafuko.
Wakati huo huo, Mwachiro Diyo, mmoja wa wanafamilia ya Mwachizi, amethibitisha kuwa familia hiyo iliuza shamba hilo kwa Saidi Nzuga na Fred Kanato.
Diyo amesema shamba hilo lilikuwa mali ya familia ya Mwachizi kwa muda mrefu na kwamba mauziano hayo yalifanyika kwa njia halali.
Mwanafamilia mwingine, Ngumi Kombo, pia amethibitisha kuwa familia hiyo iliuza shamba hilo kwa Nzuga na Kanato kutokana na hali ngumu ya maisha.
Kombo amesema kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, Saidi Nzuga na Fred Kanato ndio wamiliki halali wa shamba hilo, na amewataka watu wanaodai kuwa ardhi hiyo ni mali yao kuondoka kwa amani ili kuepusha mzozo au makabiliano.
Comments
Post a Comment