KTDA Yasafirisha Tani 99,000 za Mbolea kupitia SGR Kuwafikia Wakulima wa majani Chai.
Shirika la KTDA limeanza kusafirisha tani 99,000 za mbolea kutoka Bandari ya Mombasa hadi Nairobi kupitia reli ya kisasa (SGR), kwa ajili ya usambazaji kwa wakulima wa majani chai nchini.
Mwenyekiti wa Kitaifa wa KTDA, Enos Njeru EGH, amesema shehena hiyo imeagizwa kupitia zabuni ya kimataifa kwa niaba ya zaidi ya wakulima 650,000. Meli ya kwanza kati ya tatu imewasili Mombasa Septemba 3, huku mbili zikitarajiwa kufika ndani ya mwezi huu.
Baada ya kufungashwa, shehena hiyo itazalisha takribani mifuko milioni 1.9 ya mbolea aina ya NPK 26:5:5, kila mmoja ukiwa na uzito wa kilo 50. Kiasi hicho kimeongezeka kutoka tani 93,000 mwaka 2023.
Njeru amesema matumizi ya SGR yatawezesha mbolea kusafirishwa kwa haraka na kwa ufanisi kutoka Mombasa hadi Nairobi, kabla ya kusafirishwa kwa barabara hadi viwandani ambako itagawiwa kwa wakulima walioagiza.
Amesema shirika la KTDA linalenga kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa wakati, hasa msimu wa mvua unapokaribia, huku maafisa wa nyanjani wakiwasaidia wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea.
Hata hivyo, Njeru amesema gharama ya mbolea imeathiriwa na mambo ya kimataifa, yakiwemo gharama ya gesi asilia, mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha, usafirishaji, bima na hali ya soko la kimataifa.
Amesema gharama hiyo imefika zaidi ya Sh5,500 kwa mfuko wa kilo 50 kutokana na changamoto za bei na usafirishaji, huku gharama ya mwisho kwa mkulima ikitegemea pia gharama za usafirishaji, uondoaji bandarini na bima.
KTDA imeitaka Serikali kuendeleza ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa majani chai, ikisema mpango huo umewasaidia kupata mfuko wa kilo 50 kwa Sh2,500 kwa miaka mitano iliyopita.
Njeru ameomba wakulima wa majani chai wapewe ruzuku sawa na ile iliyoahidiwa kwa wakulima wa mazao mengine, ambapo mfuko wa kilo 50 unalengwa kuuzwa kwa Sh2,000.
Aidha, ameomba Serikali kulipa madeni ya ruzuku ambayo hayajalipwa kutoka miaka iliyopita, akisema mzigo huo unaendelea kuwaathiri wakulima kutokana na riba. KTDA imesema itaendelea kutafuta njia za kupunguza gharama za uzalishaji na kuwaweka wakulima mbele.
Comments
Post a Comment