Kaunti ya Mombasa kunufaika na Miradi ya Nyumba za Bei Nafuu ya Bilioni 30.

                          


Kaunti ya Mombasa inatarajiwa kunufaika na miradi ya nyumba za bei nafuu yenye thamani ya takriban Shilingi Bilioni 30, hatua inayolenga kubadilisha sura ya jiji hilo la kitalii na kuhakikisha wakazi wanapata makazi ya kisasa na yanayomudu gharama.

Akizungumza mjini Mombasa wakati wa zoezi la kupeana ufahamu Kwa jamii kuhusu mradi wa nyumba za bei nafuu Mkurugenzi wa Uratibu wa Kanda ya Pwani, Idara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji John Karanja, amesema serikali inawekeza katika miradi ya nyumba za bei nafuu, masoko na hosteli za wanafunzi ili kukabiliana na uhaba wa makazi jijini Mombasa.

                                 

Karanja amesema nyumba hizo zitawanufaisha maelfu ya watu wanaofanya kazi Mombasa lakini hulazimika kuutafuta makazi katika Kaunti jirani.

Miongoni mwa miradi hiyo ni Mradi wa Nyumba za Bei Nafuu wa Nyali, wenye thamani ya bilioni 6 na unaotarajiwa kujenga nyumba 2,220.

Mradi wa Nyumba za Bei Nafuu wa Changamwe NHC, wenye thamani ya Shilingi bilioni 5,Mradi wa Nyumba za Bei Nafuu wa Makupa, wenye thamani ya Sh6.9 bilioni,Miradi mingine ni pamoja na Port Reitz Student Accommodation Units, ambao unaendelea, Shanzu Hostels, Mradi wa Nyumba wa Hobley wenye thamani ya Sh4.5 bilioni pamoja na Sega MUD.

                                         

Kwa upande wake mkurugenzi wa Nyumba za bei nafuu Kaunti ya Mombasa, Meshack Otieno, amewahimiza wakazi kujisajili katika mpango wa Boma Yangu ili kunufaika na nyumba za bei nafuu zinazojengwa katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.

Otieno amewapa wakazi maelezo kuhusu mchakato wa kujisajili, kupata nyumba na kufanya malipo, akisisitiza umuhimu wa kuanza mchakato mapema.

Amesema ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika eneo la VOK na unatarajiwa kukamilika Machi 2027, huku Hobley Estate ikiwa na nyumba 1,752 zinazoendelea kujengwa.

                                 

Otieno amesema nyumba hizo zinalenga wananchi wanaokidhi vigezo, akiwataka wanaotaka kunufaika kujisajili na kuanza kufanya malipo kwa wakati.

Mbunge wa Mvita, Mohamed Sudi Machele, amewataka wakazi wa eneo hilo kuchangamkia mpango wa serikali wa nyumba za bei nafuu kupitia mradi wa Boma yangu, akisema takriban nyumba 1,800 zinatarajiwa kujengwa katika eneo hilo.

Machele amesema ameandaa zoezi maalum la kuwaelimisha wakazi kuhusu namna ya kutuma maombi na kunufaika na nyumba hizo, akisema wengi bado hawajafahamu mchakato huo. Amesema mradi wa Makupa Market utakuwa na soko pamoja na nyumba za makazi.

Amesema mipango mingine inalenga Old Town, ambako kutajengwa soko la samaki la ghorofa tatu pamoja na nyumba za makazi. Ameongeza kuwa miradi hiyo itatekelezwa kwa awamu, huku kila mradi ukiwa na mkataba na muda wake wa kukamilika.

Machele amesema wanufaika hawatalazimika kulipa gharama yote ya nyumba mara moja, bali watalipa amana na kuendelea na malipo kwa utaratibu uliowekwa hadi kumiliki nyumba.

                        

Mbunge huyo amewataka wakazi kuacha kupinga mradi huo kwa misingi ya kisiasa, akisema wanapaswa kuangalia manufaa yake kwa wananchi badala ya kuhusisha mradi na Rais William Ruto.

Amesema Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeshirikiana na Serikali ya Kitaifa kwa kutoa ardhi kwa ajili ya miradi hiyo, huku akisisitiza kuwa nyumba zote haziwezi kutolewa kwa wananchi kwa wakati mmoja kwa sababu mpango huo ni wa muda mrefu.

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.