Wakazi wa Lamu Wataka Asilimia 70 ya Ajira Katika Mradi wa Kusafisha Mafuta wa Dangote.

        

Wakazi wa kaunti Lamu wameitaka Serikali kuhakikisha jamii inashirikishwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi wa kusafisha mafuta, wakisisitiza kuwa ushirikishwaji huo ndio utakaowezesha wananchi kunufaika na mradi huo.

Wakizingumza na waandishi wa habari wakiongozwa na Sultan Omar Sharif amesema wakaazi wameupokea na kuukaribisha mradi huo, ila wanataka kushirikishwa kwa asilimia 100 kuanzia hatua za upangaji hadi utekelezaji.

Amesema vijana wa eneo hilo wanahitaji kupewa kipaumbele katika ajira, akitaka asilimia 70 ya nafasi za kazi zitakazozalishwa na mradi huo zitolewe kwa wenyeji pamoja na kupewa mafunzo ya kuwajengea uwezo.

Aidha, ametaka asilimia mbili ya faida ya mradi irejeshwe kwa jamii kupitia mfuko wa maendeleo utakaosaidia kuboresha huduma mbalimbali na miundo mbinu. 

Kwa upande wake, Bado Somo amesema makubaliano kuhusu manufaa ya mradi yanapaswa kuwekwa wazi na kuandikwa rasmi badala ya kutolewa katika majukwaa ya kisiasa. 

       

Amesema wananchi wanataka kufahamu namna Kaunti ya Lamu na jamii zinazozunguka mradi zitakavyonufaika.

Naye Abubakar Bausi amesema wananchi wa Lamu wamechoshwa na ahadi zisizotekelezwa kuhusu miradi mikubwa, akidai kuwa katika miradi kama ule wa LAPSSET, wengi wa wakaazi hawakupata ajira wala kunufaika na maendeleo ya miundombinu. 

Amedai nafasi nyingi za kazi zilipewa watu kutoka nje ya eneo hilo huku baadhi ya viongozi wakituhumiwa kuuza fursa hizo. Amesisitiza kuwa safari hii wananchi hawatakubali kutengwa na maamuzi yanayohusu mradi huo, wakitaka pia fidia ya haki kwa ardhi itakayotumika.

Kwa upande wake, Alawi Abzein amesema ni muhimu kampuni inayotekeleza mradi huo kukutana moja kwa moja na wananchi badala ya kutegemea viongozi wa kisiasa pekee.

Amesema wananchi wanahitaji kufahamu athari za mradi kwa mazingira na jamii, namna fidia itakavyotolewa, pamoja na kuanzishwa kwa mfuko maalum wa maendeleo ya jamii utakaowanufaisha wakazi wa eneo hilo.

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.