Starehe Bikeathon Yawasili katika kaunti ya Mombasa Baada ya Safari ya Kilomita 1,100.
Safari hiyo ilipitia maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo Bonde la Ufa, Nairobi, maeneo ya ukambani na milima ya Taita Taveta, kabla ya kufikia jiji la Mombasa. Waendesha baiskeli hao walipokelewa kwa shangwe na wafadhili wakuu wakiongozwa na Safaricom, St. John’s Ambulance na Vivo Energy.
Tukio hilo linalojulikana kama Dr. Geoffrey Griffins Memorial Charity Bikeathon 2026, lilianza tarehe 3 Agosti mjini Busia kwa lengo la kukusanya zaidi ya shilingi milioni 10 zitakazotumika kusaidia wanafunzi wa Starehe Boys’ na Starehe Girls’ schools.
Kiongozi wa kiufundi wa timu hiyo, Ian Hisho, amesema tayari wamefanikiwa kukusanya asilimia 10 ya lengo lao la shilingi milioni 10. Akisema wana matumaini ya kufikia lengo hilo kabla ya uzinduzi rasmi wa mpango huo mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa upande wake, Leon Stanley, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Starehe Boys Centre aliyeshiriki safari hiyo, amesema changamoto kubwa walikumbana nayo ilikuwa msongamano wa magari, hasa katika barabara ya kutoka Nairobi hadi Mombasa.
Amesema ukosefu wa njia maalumu za waendesha baiskeli ulifanya sehemu hiyo ya safari kuwa ngumu, huku akiitaka serikali kuweka miundombinu salama kwa waendesha baiskeli.
Mwakilishi wa Vivo Energy, Sarah Mucina, amesema kampuni hiyo ilichangia katika safari hiyo kwa kutoa mahitaji mbalimbali, ikiwemo vinywaji na viburudisho kuanzia Busia hadi Mombasa. Amesema kampuni hiyo inaendelea kuweka mkazo kwa vijana kwa kuwa ndio viongozi wa taifa la kesho.
Bikeathon hiyo ni ya pili kuandaliwa na wanafunzi wa sasa na waliowahi kusoma katika shule ya Starehe Boys Centre kwa lengo la kuwahamasisha wafadhili na wasamaria wema kuchangia mfuko wa pamoja wa kusaidia wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo katika shule hizo mbili za Starehe Boys’ na Girls’.
Zaidi ya wanafunzi 15 na waliowahi kuwa wanafunzi wa Starehe walishiriki katika safari ya mwaka huu.



Comments
Post a Comment