Serikali Yashinikizwa Kutunga Sheria kudhibiti swala la watu Kutoweka
Wanaharakati wa haki za binadamu na mashirika ya kiraia wametoa wito kwa Serikali na Bunge kutunga sheria inayotambua na kuifanya kuwa kosa la jinai vitendo vya watu kutoweka nchini Kenya.
Wito huo umetolewa wakati wa hafla ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya uhamasishaji kuhusu watu wanaotoweka, huku wadau wakitaka hatua zaidi zichukuliwe kulinda waathiriwa na familia zao.
Wangeshi Grace Kahuria kutoka IMLU, ambaye pia ni mwanachama wa Muungano wa Missing Voices Coalition na mratibu wa Police Reforms Working Group, amesema mamia ya visa vya watu waliopoteza maisha au kutoweka vimeripotiwa nchini kwa miaka kadhaa.
Kahuria amesema visa 38 viliripotiwa mwaka 2019, 10 mwaka 2020, 36 mwaka 2021, 22 mwaka 2022, 10 mwaka 2023, zaidi ya 50 mwaka 2024 na visa sita mwaka 2025.
Amesema hadi kufikia Agosti mwaka huu, visa 19 tayari vimeripotiwa.
Kahuria amesema familia za watu waliotoweka au wale ambao miili yao imepatikana baada ya kuuawa zinaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za kihisia na kifedha huku serikali bado ikiwa haijawapatia fidia.
Ametaka kukomeshwa kabisa visa vya watu kutoweka, huku akitaka Serikali kutoa huduma na msaada kwa familia zilizoathiriwa na vitendo vya ukatili.
Aidha, ameitaka Serikali kuacha mashirika kama Kenya National Commission on Human Rights pamoja na Victims Protection Agency kufanya kazi huru ili taasisi hizo ziweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuwasaidia waathiriwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa shirika la MUHURI, Khelef Khalifa,amekosoa matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia na kutaka maafisa wa polisi wawajibishwe kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Khalifa pia amekosoa kauli ya Rais William Ruto kuhusu polisi kuwapiga risasi waandamanaji miguuni, kuwapeleka hospitalini na kisha kukabiliwa na kifungo.
Akisema kauli kama hiyo zinaweza kuchochea matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wasio na silaha.
“Rais amekosea. Anawahimiza polisi kutumia nguvu na kuwaua raia wasio na silaha,” amesema Khalifa.
Amesema watu waliotoweka wanapaswa kutafutwa na waliohusika na kutoweka kwao kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akisisitiza kuwa mtu anayeshukiwa kufanya uhalifu anapaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani, badala ya polisi kuchukua sheria mikononi mwao.
“Ikiwa mtu amefanya uhalifu, anapaswa kufikishwa mahakamani na mahakama ndiyo iamue hatua ya kuchukuliwa dhidi yake. Si jukumu la polisi kuchukua sheria mikononi mwao,” amesema.
Aidha, amewataka maafisa wa polisi kuacha kutumiwa kisiasa na badala yake kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
“Polisi wanapaswa kuacha kufuata wanasiasa. Wajibu wao ni kufanya kazi kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Nae Mkurugenzi wa International Justice Mission (IJM) nchini Vincent Chahale, amesema siku hiyo ni muhimu katika juhudi za kukabiliana na tatizo la watu kutoweshwa kwa kulazimishwa nchini.
Chahale ametangaza kuzinduliwa kwa kampeni ya “Haki Kwa Wote”, inayolenga kushinikiza mageuzi ya kisheria na kitaasisi ili kulinda waathiriwa na familia zao.
Amesema kampeni hiyo inalenga mambo mawili makuu; kwanza, kushinikiza Serikali na Bunge kutunga sheria inayofanya kutoweka kwa kulazimishwa kuwa kosa la jinai.
Pia kampeni hiyo inalenga kuhakikisha sheria hiyo inapitishwa ifikapo katikati ya mwaka ujao.
“Kwa miaka mingi tumekuwa na visa vya watu kutoweka, hasa wakati wa uchaguzi na maandamano, lakini bado hatuna sheria inayofanya kitendo hicho kuwa kosa la jinai,” amesema Chahale.
Lengo la pili la kampeni hiyo ni kuhakikisha utekelezaji kamili wa Sheria ya Ulinzi wa Waathiriwa (Victim Protection Act).
Akisema hakuna maana ya kuwa na sheria ambayo haitekelezwi ipasavyo.
Kampeni ya Haki Kwa Wote inawaleta pamoja wadau wa haki za binadamu na washirika wengine wanaotaka kuona uwajibikaji zaidi, haki na ulinzi kwa waathiriwa wa kutoweka pamoja na familia zao.
Wadau hao wamesema Serikali inapaswa kuimarisha mifumo ya kisheria na taasisi ili kuhakikisha waathiriwa wanapata haki na waliohusika na ukiukaji wa haki za binadamu wanawajibishwa.



.jpeg)
Comments
Post a Comment