MOMBASA MEGA MARATHON: KITUNDU NA CHERUIYOT WASHINDA MBIO ZA KILOMITA 42.
Mwanariadha Little Nick Kitundu ameibuka mshindi wa mbio za kilomita 42 katika Mombasa Mega Marathon, baada ya kutumia muda wa saa 2:16:02.
Kitundu alifuatwa na Gabriel Kahora, aliyemaliza katika
nafasi ya pili kwa muda wa saa 2:18:39,
huku Theophilus Kipsang akimaliza wa tatu kwa muda wa saa 2:18:54.
Kwa upande wa wanawake katika mbio za kilomita 42, Betty
Cheruiyot alitwaa ushindi kwa muda wa saa
2:36:09. Akifuatwa na Lucy Chelele, aliyemaliza wa pili kwa muda wa saa 2:40:59, huku Anastacia Jepkoech akishika
nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:42:27.
Katika mbio za kilomita 21 upande wa wanaume, Justus Muasya
alishinda kwa muda was aa 1:00:52, akifuatiwa na Elisha Kipsoi aliyemaliza wa
pili kwa muda wa saa 1:02:55 nae Tom Mwendwa Mutie akishika nafasi ya tatu kwa
muda wa 1:05:57.
Akizungumza baada ya ushindi wake, Little Nick Kitundu
amesema mbio hizo hazikuwa rahisi kutokana na hali ya hewa ya joto, lakini amefurahia
kufanikiwa kushinda. Akisema alifurahishwa na mazingira tambarare ya
Mombasa, kwani amezoea kukimbia katika maeneo yenye milima na mabonde.
Kwa upande wake, Betty Cheruiyot amesema hali ya hewa
ilikuwa changamoto kubwa, lakini haikumzuia kufanya vizuri na kutwaa ushindi.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Mombasa Mega Marathon,
Charles Omoto, ameipongeza Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano wake katika
kufanikisha mbio hizo. Omoto akisema waandalizi wanapanga kufanya mashindano
hayo kuwa ya kila mwaka, kutokana na vipaji vingi vilivyojitokeza.
Waziri wa Ardhi na Mipango ya Jiji katika Kaunti ya Mombasa,
Mohamed Husein Amadoh, amewataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za
kulevya na badala yake kujikita katika michezo kama njia ya kuimarisha afya na kujenga
maisha bora.
Amadoh amesema Mombasa Mega Marathon haikuwa tukio la
michezo pekee, bali pia ilikuwa jukwaa la kuhamasisha umoja, maisha yenye afya
na kujenga kizazi kisichotumia dawa za kulevya. Amewataka vijana kutumia fursa
zinazopatikana kupitia michezo kugundua na kuendeleza vipaji vyao, kutafuta
fursa za maendeleo na kufanya maamuzi yenye manufaa kwa maisha yao.
Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Sharif Nassir,
amewapongeza waandalizi wa mbio hizo akisema wametanya kazi nzuri katika
kuwasaidia vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kujenga maisha
bora kupitia hamasa yao.
Gavana Nassir amesema mbio hizo pia zimechangia pakubwa
katika kukuza na kutangaza utalii wa kaunti ya Mombasa kupitia maonyesho ya
maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.
Aidha, amewataka wanasiasa kujiepusha na kauli zinazoweza
kuathiri sekta ya utalii, akisema kuathirika kwa utalii kunaweza kudhoofisha
uchumi na kusababisha Wakenya wengi kukosa ajira.
Gavana Nassir amesema serikali ya kaunti itaendelea
kuboresha mbio hizo ili ziwe kubwa, za kuvutia na zenye manufaa zaidi katika
miaka ijayo.
Akiweka wazi kuwa Mombasa imepiga hatua kubwa katika sekta ya
michezo, huku viwanja vya kisasa vikiendelea kujengwa ili kuendelea kutambua na
kukuza vipaji.
Mshindi wa mbio za kilomita 42 amejishindia zawadi ya shilingi 500,000, mshindi wa pili shilingi 250,000, huku mshindi wa tatu akipata shilingi 125,000. Zawadi zilitolewa hadi kwa mshindi wa nafasi ya kumi




Comments
Post a Comment