Gavana Abdulswamad Awataka Vijana Kukataa Siasa za Chuki na Ubaguzi.
Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir, amewataka vijana kuachana na wanasiasa wanaoendeleza siasa za chuki na ukabila kuwagawa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani, Gavana Abdulswamad amesema vijana wanapaswa kusikiliza sera za kila mwanasiasa na kutathmini namna anavyolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Mombasa.
Abdulswamad akiwataka vijana kuacha kufuata wanasiasa wasio na ajenda wala maono ya kubadilisha maisha yao, akisisitiza umuhimu wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia sera na mipango ya maendeleo.
Gavana amesema ukosefu wa ajira ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili vijana nchini, na serikali ya kaunti ya Mombasa imeweka mikakati mbalimbali ya kuwawezesha vijana kujikimu kimaisha.
Aidha, amewataka vijana kuwa na nidhamu na kujituma katika kazi, akisema baadhi yao walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika mpango wa Mombasa Ni Yangu, jambo lililoathiri utekelezaji wa mradi huo.
Gavana Abdulswamad amesema ndani ya wiki mbili zijazo programu ya Skills Mtaani itaanza rasmi, huku akihakikisha kuwa hakuna kijana atakayeachwa nje, kwani utaratibu maalum tayari umewekwa.
Amesema vijana watakaopata fursa ya kusomea kozi mbalimbali watanufaika na fedha maalum za mfuko wa hazina ya pesa ya mikopo utakaowasaidia kupata vifaa vya kuanzisha biashara zao baada ya mafunzo.
Biashara hizo, amesema, zitasaidia pia kuunda nafasi za ajira kwa vijana wengine na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mombasa.
Gavana pia amewakosoa wapinzani wanaoendeleza siasa za chuki na ubaguzi, akiwataka viongozi kujenga jamii yenye amani, umoja na upendo.
Wakati huo huo, ameagiza jopokazi linaloshughulikia masuala ya vipaji katika Kaunti ya Mombasa kuandaa tamasha maalum litakalolenga kutambua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana.
Comments
Post a Comment