Zaidi ya familia 800 zaachwa bila makazi baada ya Nyumba 170 Kubomolewa Changamwe.
Viongozi hao wakiongozwa na Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi wakisema hatua hiyo ilifanyika licha ya kuwepo kwa amri ya mahakama kuzuia ubomozi. Viongozi hao wameonya kuwa uongozi wa ODM unaweza kutathmini upya uungaji mkono wake kwa serikali ya ushirikiano mpana (Broad-Based Government) kutokana na kile walichokitaja kuwa ni kupuuzwa kwa utawala wa sheria.
Zaidi ya familia 800 zilivamiwa na msafara mkubwa wa maafisa wa polisi alfajiri ya leo wakati serikali ikianza utekelezaji wa mpango wa kubomoa nyumba hizo ili kupisha mradi wa ujenzi upya wa makazi hayo.
Juhudi za viongozi wa eneo hilo kuwasihi polisi wawape wakazi muda wa kuokoa mali zao hazikufaulu, huku tingatinga likianza kubomoa nyumba hizo na kuwaacha wakaazi bila usaidizi.
Wakati huo huo, polisi wa kutuliza ghasia walirusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wakazi pamoja na viongozi waliokuwa wakipinga ubomoaji huo.
Mbunge wa Changamwe, Omar Mwinyi, amesema maafisa wa Shirika la Taifa la Nyumba walitoa notisi ya mwezi mmoja ya kuhama bila kuwashirikisha viongozi wa eneo wala kufanya ushirikishwaji wa umma.
"Tulitaka mazungumzo lakini walikataa. Tulienda mahakamani mara mbili na tukapata amri za kusitisha ubomoaji," amesema Mwinyi.
Ameweka wazi kuwa wapangaji 34 walilipwa fedha za kuhamia makazi mengine kati ya shilingi 4,000 na 10,000, kiasi alichokitaja kuwa ni kidogo mno na dharau kwa wakazi ambao wengi wameishi katika makazi hayo kwa zaidi ya miaka 30.
Mbunge huyo amesema wakazi walipaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato huo, akibainisha kuwa watoto wengi wanasoma katika shule za jirani na kuwa ubomoaji wa ghafla utavuruga masomo yao, hasa wanaojiandaa na mitihani ya kitaifa.
Aidha, amewashutumu polisi kwa madai ya kuwasili na watu aliowaita wahuni kutoka eneo jirani, akidai kuwa baadhi yao waliiba mali za wakazi kabla ya kukamatwa na kushambuliwa na wananchi wenye hasira.
"Tuliamini kuwa katika serikali ya ushirikiano mpana tungehusishwa na kushauriwa kuhusu masuala yanayohusu maeneo yetu. Lakini kinachoendelea kinaonyesha huenda bado tuko upinzani. Kama tungekuwa serikalini, tusingeadhibiwa pamoja na wananchi wetu," amesema Mwinyi.
Kwa upande wake, Seneta wa Mombasa Mohamed Faki ameema ni jambo la kushangaza kuwa Kenya ni miongoni mwa nchi zilizotia saini mikataba ya kimataifa inayopinga uhamishaji wa watu kwa nguvu, lakini bado wakazi walifurushwa licha ya kuwepo kwa amri halali ya mahakama.
"Ikiwa Shirika la Taifa la Nyumba liko juu ya sheria, wananchi waambiwe. Ikiwa Polisi wako juu ya sheria, hilo pia lielezwe, kwa sababu haiwezekani amri ya mahakama ipuuzwe," amesema Faki.
Ameongeza kuwa mamlaka husika zilipaswa kushirikisha viongozi wa eneo hilo ili kupata suluhisho la maelewano badala ya kutumia nguvu.
Mwenyekiti wa wapangaji, Meshack Okeyo, amesema wakazi hawapingi miradi ya maendeleo ya serikali, akieleza kuwa walikuwa wamekubaliana na maafisa wa Idara ya Makazi kusitisha notisi za kuhama, lakini walishtuka kuamka na kukuta polisi wakisimamia ubomoaji huo.
"Tunaunga mkono miradi ya serikali, lakini uhamishaji wa wananchi unapaswa kufanyika kwa njia ya kibinadamu. Zoezi hili lisitishwe ili mazungumzo yafanyike. Hatutaki mtu yeyote aumie," alisema Okeyo.
Comments
Post a Comment