WAZIRI JOHO ASITISHA SHUGHULI ZA UCHIMBAJI MADINI ZA KAMPUNI YA TATA CHEMICALS MAGADI LIMITED

               

Waziri wa Madini, Uchumi samati na Masuala ya Bahari, Hassan Ali Joho, ameagiza kusitishwa mara moja kwa shughuli zote za uchimbaji madini za kampuni ya Tata Chemicals Magadi Limited hadi pale itakapotekeleza kikamilifu matakwa ya Sheria ya Madini, kanuni zake na sheria nyingine zote zinazosimamia sekta ya madini nchini Kenya.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya miaka kadhaa ya mazungumzo kati ya Idara ya Serikali ya Madini na Tata Chemicals Magadi Limited kuhusu wajibu wake wa kisheria chini ya Sheria ya Madini, kifungu cha 306, Kanuni za Leseni na Vibali vya Madini za mwaka 2017, Kanuni za Ukusanyaji na Usimamizi wa Mrabaha wa Madini za mwaka 2024 pamoja na mifumo mingine ya kisheria inayohusika.

Licha ya mazungumzo hayo, masuala kadhaa muhimu ya uzingatiaji wa sheria bado hayajatatuliwa. Miongoni mwao ni ukosefu wa mkakati wa wazi wa uongezaji thamani wa madini, madeni ya upatanisho na malipo ya mrabaha, upungufu katika utoaji wa taarifa na upatanisho wa mauzo ya nje, utekelezaji duni wa Makubaliano ya Maendeleo ya Jamii (CDA), kutokuwepo kwa mpango wa kutosha wa ajira na uhamishaji wa ujuzi kwa Wakenya, matumizi hafifu ya bidhaa na huduma za ndani pamoja na mapungufu katika utekelezaji wa masharti ya mazingira.

Kutokana na hali hiyo, kampuni imeagizwa kuwasilisha nyaraka zote muhimu na ushahidi unaothibitisha kuwa imetekeleza kikamilifu wajibu wake wa kisheria na kushughulikia madeni au wajibu wowote uliosalia kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli za uchimbaji.

Waziri Joho amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kuhakikisha rasilimali za madini nchini zinatumika kwa uwajibikaji, kwa njia endelevu na kwa manufaa makubwa ya kiuchumi kwa taifa, huku ikilinda mazingira na maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji.

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.