Wakazi wa Lamu Wataka Kushirikishwa Katika Mradi wa Kituo cha Kusafisha Mafuta Cha Bilionea Dangote.
Wakazi na viongozi wa Kaunti ya Lamu wameitaka Serikali kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa kituo cha kusafisha mafuta chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 kwa siku, unaotarajiwa kujengwa na kampuni ya mfanyabiashara Aliko Dangote.
Wakiongozwa na Sultan Omar Sharif, viongozi hao wamesema hawapingi mradi huo, bali wanataka Serikali iwe wazi na kuwahusisha wakazi wa eneo hilo katika kila hatua ya utekelezaji ili kuhakikisha wanapata manufaa ya moja kwa moja.
Sultan Sharif amesisitiza kuwa ajira zinazotarajiwa kufunguliwa kupitia mradi huo, zinazokadiriwa kufikia zaidi ya nafasi 60,000 na zinapaswa kutanguliza wakazi wa Lamu.
Aidha, ameitaka kampuni husika kutekeleza miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) ikiwemo ujenzi wa shule, barabara na miundombinu mingine muhimu ili kuboresha maisha ya wananchi.
Ameongeza kuwa mradi huo una uwezo wa kuibadilisha kwa kiasi kikubwa hali ya uchumi wa Kaunti ya Lamu ikiwa utekelezaji wake utazingatia maslahi ya wananchi wa eneo hilo.
Wanajamii hao pia wamemwomba Rais William Ruto kusikiliza kilio cha wakazi wa Lamu na kuhakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika maamuzi yanayohusu mradi huo mkubwa.
Kwa upande wake, Kijana Athuman Mohamed Abubakar amesema wanaunga mkono ujio wa mradi huo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwazi na ushirikishwaji wa jamii katika uundaji wa sera na mipango itakayowezesha wananchi kufaidika.
Naye Mohamed Twalib amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii ikiwa utasimamiwa kwa usawa.
Akipendekeza kuwa angalau asilimia 70 ya nafasi za ajira zitolewe kwa wakazi wa Lamu, huku biashara ndogo ndogo zinazohusiana na shughuli za kiwanda hicho ikiwemo usambazaji wa vifaa na huduma mbalimbali, zipewe kipaumbele kwa wafanyabiashara wazawa.
Akiongeza kuwa Sultan Omar Sharif ahusishwe katika masuala yote yanayohusu mradi huo kwa niaba ya jamii.
Haula Issa naye ametaka mradi huo utoe fursa za kweli kwa vijana wa Lamu, akisema hawataki kurudia hali iliyoshuhudiwa katika miradi mingine ambapo wananchi wa eneo hilo hawakunufaika ipasavyo.
Mradi huo wa kituo cha kusafisha mafuta wenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 kwa siku unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha takribani miezi 30.
Comments
Post a Comment