Wahudumu wa Bodaboda Watakiwa Kudumisha Usalama na Kuweka Akiba kwa Mustakabali Bora wa maisha ya baadae.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa Wahudumu wa Bodaboda, Kevin Mubadi, amewataka wahudumu wa bodaboda kote nchini kudumisha usalama na kutumia fursa za uwezeshaji wa kiuchumi ili kuboresha maisha yao.
Akizungumza wakati wa mkutano na wahudumu wa bodaboda jijini Mombasa, Mubadi amesema kuwa mipango ya kuwawezesha vijana kupata pikipiki kupitia mikopo imechangia kupunguza uhalifu na kuimarisha usalama, kwani wengi wao wanapata kipato halali badala ya kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.
Amepongeza mashirika mbalimbali yanayoshirikiana na sekta ya bodaboda kwa kuwawezesha vijana kupata pikipiki kwa njia ya mikopo, akisema hatua hiyo imewapa fursa ya kujitegemea na kupunguza idadi ya vijana wanaojiunga na makundi ya uhalifu.
Mubadi pia amewasihi wahudumu wa bodaboda kutoruhusu kutumiwa vibaya na wanasiasa kuelekea katika kipindi hiki Cha uchaguzi.
Amewataka kujiepusha na vurugu na vitendo vya kihuni, badala yake washirikiane kwa karibu na vyombo vya usalama na kuwa mstari wa mbele kuripoti matukio yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama wa wananchi.
Aidha, amewashukuru wahudumu wa bodaboda kwa kutoshiriki katika maandamano yaliyoshuhudiwa nchini katika siku za hivi karibuni, akiwahimiza kuendelea kuwa mabalozi wa amani.
Mwenyekiti huyo pia amewataka wahudumu wa bodaboda kujiepusha na tabia za kuchoma magari au kuharibu mali wakati ajali zinapotokea, akisisitiza kuwa wanapaswa kuziachia mamlaka husika zifuate taratibu za kisheria badala ya kuchukua sheria mikononi mwao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wahudumu wa Bodaboda Kaunti ya Mombasa, Samuel Ogutu, ameshukuru mashirika mbalimbali kwa kushirikiana na sekta hiyo kwa kutoa huduma mbalimbali zinazohusiana na pikipiki bila malipo, hatua ambayo amesema imewapunguzia wahudumu wa bodaboda gharama za uendeshaji.
Ogutu akitoa wito kwa mashirika hayo kuendelea kuandaa shughuli kama hizo mara kwa mara ili kupata nafasi ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wahudumu wa bodaboda na kutafuta suluhisho la pamoja.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kenya National Entrepreneurs Saving Trust KNEST, Lucy Kamau, amewahimiza wahudumu wa bodaboda kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Lucy amesema waendesha bodaboda wanaweza kuanza kuweka akiba kidogo kidogo kwa siku, akieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia kujitegemea kifedha badala ya kutegemea msaada wa serikali au familia wakati wa uzeeni au wanapopatwa na dharura.
Amesema KNEST, ambayo ilizinduliwa mwezi Desemba mwaka jana, tayari imeandikisha zaidi ya wanachama milioni 1.5 nchini na imepokelewa vyema na Wakenya kutokakana na huduma zake nzuri.
Ameeleza kuwa lengo la mpango huo ni kuhakikisha wananchi wanapata hifadhi ya kifedha wanapostaafu au wanapofikia umri wa uzee.
Ameongeza kuwa wanachama wanaweza kupata hadi asilimia 30 ya fedha walizowekeza pale wanapokumbwa na dharura, huku fedha zilizosalia zikiendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya mafao ya baadaye.
.jpeg)



Comments
Post a Comment