Serikali ya kaunti ya Mombasa Yazindua Kozi Mpya Kuimarisha Uchumi wa Bahari na Ajira kwa Vijana
Serikali ya Kaunti ya Mombasa imezindua kozi mpya za mafunzo ya ufundi katika chuo cha Ufundi cha Mtongwe kwa lengo la kuwapa vijana ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kupata ajira katika sekta ya uchumi samawati na maeneo mengine yanayokua kwa kasi pamoja na kituo cha kulelea watoto na maeneo ya michezo ili kuwasaidia wazazi vijana, hususan akina mama, kuendelea na masomo yao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdullswamad Sheriff Nassir amesema serikali ya kaunti imejizatiti kuhakikisha mafunzo ya ufundi yanakuwa njia ya moja kwa moja kuelekea ajira kwa kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi pamoja na kupanua programu za ukuzaji wa ujuzi.
Akisema kuwa vyuo vyote vya ufundi vinavyotaka kushirikiana na serikali ya kaunti vitakutana wiki hii katika eneo la Tononoka ili kuandaa mfumo wa kuwaandaa vijana kwa ajira kupitia programu za maendeleo ya ujuzi katika jamii "SKILLS MTAANI".
Abdulswamad pia ameagiza Idara ya Elimu kuhakikisha wanafunzi wa Mombasa wanapewa kipaumbele katika vyuo vya ufundi vya kaunti na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuweka mafunzo hayo karibu na wananchi na kwa gharama nafuu.
Akiweka wazi kuwa wahitimu wa vyuo vya ufundi vya kaunti watapewa kipaumbele katika nafasi za mafunzo kwa vitendo (attachments), mafunzo kazini (internships) na ajira ndani ya serikali ya kaunti pale nafasi zitakapopatikana.
Gavana huyo akisema kuwa serikali ya kaunti itashirikiana na kampuni binafsi ili kuajiri wahitimu hao, huku ikichunguza uwezekano wa kutoa motisha kwa kampuni zitakazoajiri vijana waliopata mafunzo katika vyuo vya Mombasa.
Kwa wahitimu watakaochagua kujiajiri, gavana amesema hazina ya pesa ya mikopo ya mzunguko (Mombasa County Revolving Fund) utawasaidia kwa kugharamia ununuzi wa zana na vifaa muhimu vya kuanzisha biashara zao.
Kwa upande wake waziri wa elimu katika kaunti ya Mombasa Dkt. Mbwarali Kame, amesema kaunti inalenga kuvifanya vyuo vya ufundi kuwa vituo vya ubora vinavyowaandaa vijana kwa fursa zinazotokana na uchumi wa samawati.
Amesema kozi hizo zimeandaliwa kukidhi mahitaji ya sekta zinazohusiana na usafiri wa baharini, Bandari ya Mombasa, utalii wa hoteli na huduma za baharini, ili kuhakikisha vijana ambao hawajiungi na vyuo vikuu wanapata ujuzi unaohitajika sokoni.
“Lengo letu ni kukifanya Chuo cha Mtongwe kuwa kitovu cha ubora katika mafunzo ya masuala ya baharini ili vijana wetu wanufaike na fursa za uchumi wa samawati,” amesema Dkt. Kame.
Aidha, amesema vituo vya kulelea watoto vitawasaidia akina mama vijana walioathiriwa na mimba za utotoni au ndoa za mapema kuendelea na masomo yao bila kulazimika kuyaacha
Kozi hizo mpya ni pamoja na Ujenzi na Ukarabati wa Boti, Ufundi wa Majokofu na Viyoyozi, Huduma za Malazi na Utunzaji wa Nyumba, pamoja na Teknolojia ya Uokaji Mikate na Keki.
Washikadau katika sekta ya elimu wamesema uwekezaji huo unalenga kuimarisha elimu ya ufundi, kuongeza upatikanaji wa mafunzo ya vitendo na kuunda fursa zaidi za ajira na ujasiriamali kwa vijana kote Mombasa.
Comments
Post a Comment