Serikali ya kaunti ya Mombasa kuajiri wauguzi 573 kufuatia mgomo unaondelea.
Kufuatia mgomo wa wauguzi ambao unaendelea nchini na kutatiza shughuli za utoaji huduma za afya Serikali ya kaunti ya Mombasa imetangaza zoezi la kuajiri wauguzi 573 kwa kandarasi ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kutolewa bila kukatizwa kufuatia mgomo wa kitaifa uliotangazwa na Chama cha Wauguzi Kenya (KNUN).
Akizungumza
katika mkutano na wanahabari gavana wa kaunti hiyo Abdulswamad Shariff Nassir
amewahakikishia wakazi kuwa hospitali na vituo vyote vya afya vya umma katika
kaunti hiyo vitaendelea kutoa huduma licha ya mgomo unaoendelea.
Akiwahakikishia
wakaazi wa Mombasa kuwa hakutakuwa na usumbufu wowote wa huduma za afya katika Kaunt
hiyo.
Amesema
jukumu kuu la serikali ya kaunti ni kulinda maisha ya wananchi na kuhakikisha
huduma muhimu zinaendelea kutolewa wakati wote.
"Kwa msingi
huo, nimeielekeza Bodi ya Huduma za Umma ya Kaunti kuanza mara moja mchakato wa
kuajiri wauguzi 573 kwa kandarasi ili
kuhakikisha wananchi wa Mombasa wanaendelea kupata huduma za afya bila
kukatizwa," amesema.
Abdulswamad
akisema notisi ya mgomo ilitolewa kabla ya wakati, kwa sababu wahusika wa Mkataba
wa Makubaliano ya Pamoja bado wanaendelea na mazungumzo. Akiwa na matumaini
kuwa mazungumzo hayo yatazaa suluhu ya amani itakayolinda maslahi ya wahudumu wa
afya pamoja na wananchi.
Gavana huyo
amewataka wauguzi wa Mombasa kuendelea kuwahudumia wananchi huku mazungumzo
yakiendelea, akisisitiza kuwa serikali ya kaunti inathamini mchango wao na
itaendelea kushughulikia malalamishi yao kupitia mazungumzo na taratibu za
kisheria na taasisi husika.
Abdulswamad ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Baraza la Magavana (CoG), amesema serikali za
kaunti zinatafuta mwongozo wa kisheria kuhusu notisi ya mgomo huo, akieleza
kuwa baadhi ya masuala yaliyowasilishwa na chama cha wauguzi bado yanajadiliwa
au hayako ndani ya mamlaka ya moja kwa moja ya serikali za kaunti.
Aidha,
alisema serikali ya kaunti imepokea taarifa za visa vya watu wachache
wanaodaiwa kuwahofisha wahudumu wa afya na kuwazuia wagonjwa kufika katika
vituo vya afya vya umma.
Akisema vitendo
hivyo havikubaliki, vinakiuka haki ya kikatiba ya wananchi kupata huduma za
afya, na havitavumiliwa.
Gavana akiisisitiza
kuwa uamuzi wa kuajiri wauguzi wa ziada unalenga kuhakikisha huduma za afya
zinaendelea kutolewa bila kukatizwa na haipaswi kutafsiriwa kama adhabu kwa
wahudumu wa afya.
"Hii si
hatua ya kuwaadhibu wahudumu wa afya. Ni hatua muhimu ya kuhakikisha wakazi
wanaendelea kupata huduma muhimu za afya wakati suala hili likiendelea
kushughulikiwa kupitia mazungumzo na mahakama."
Akiahidi
kuwa hakuna mgonjwa atakayekosa huduma katika Kaunti ya Mombasa kutokana na
mgomo huo uliopangwa.
Chama cha
Wauguzi nchini Kenya (KNUN) kimetoa notisi ya mgomo wa kitaifa kikieleza kuwa
kuna masuala ambayo hayajapatiwa ufumbuzi, yakiwemo utekelezaji wa Mkataba wa
Makubaliano ya Pamoja (CBA), utekelezaji wa makubaliano ya kurejea kazini ya
mwaka 2017, miongozo ya maendeleo ya kazi, kuajiriwa rasmi kwa wauguzi wa
mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC), pamoja na masuala mengine ya haki za
wafanyakazi.
Comments
Post a Comment