Pwani Innovation Week 2026 Kulenga Kuanzisha Biashara Mpya 37,000.
Pwani Innovation Week 2026 Yalenga Kuanzisha Biashara Mpya 37,000 na Kuwawezesha Vijana Milioni 2
Maandalizi ya Pwani Innovation Week 2026 yameanza rasmi huku waandalizi wakitangaza mpango kabambe wa kuanzisha biashara mpya 37,000 katika ukanda wa Pwani na kufungua nafasi za ajira kwa takriban vijana milioni mbili.
Hafla hiyo, ambayo ni makala ya saba na pia wataadhimisha miaka kumi ya kituo Cha SwahiliPot Hub Foundation, kuanzia Oktoba 26 hadi 31 ikiwakutanisha wabunifu, wajasiriamali, wawekezaji na wadau kutoka Kenya na nchi mbalimbali ulimwenguni.
Mwenyekiti wa Pwani Innovation Week, Kevit Desai, emsema tukio hilo limekuwa kichocheo muhimu cha ubunifu na ujasiriamali, likichangia kuanzishwa kwa zaidi ya biashara 4,000 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Akibainisha kuwa mwaka huu lengo ni kupanua mafanikio hayo kupitia ushauri wa kitaalamu, mafunzo, ujenzi wa mitandao na fursa za biashara kwa maelfu ya vijana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama Cha mawakili tawi la Mombasa Natasha Ali, amepongeza mchango wa SwahiliPot Hub Foundation katika kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya stadi za kazi, uongozi na ujasiriamali.
Amesema programu hizo zimewasaidia maelfu ya vijana kujijengea uwezo na kubadili taswira ya Pwani ya Kenya kuwa kitovu cha ubunifu, maendeleo na ushindani wa kiuchumi duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa kituo Cha SwahiliPot Hub Mahmoud Noor amesema taasisi hiyo imewafikia zaidi ya vijana 69,000 kupitia programu za ushauri, ukuzaji wa ujuzi na mitandao, huku zaidi ya viajana 25,000 wakipata ajira au kusaidiwa kuanzisha na kukuza biashara zao.
Noor ameongeza kuwa SwahiliPot imepanua shughuli zake kutoka Mombasa na Kilifi hadi Kitui na Nairobi kupitia ushirikiano na Mastercard Foundation pamoja na Baraza la Kitaifa la Makanisa Kenya (NCCK).
Aidha,amesema taasisi hiyo imetoa zaidi ya Shilingi milioni 1 kusaidia biashara za wanawake 108 na wajasiriamali vijana, sambamba na kuwapa ushauri na huduma za msaada wa kisaikolojia ili kuimarisha uendelevu wa biashara zao.
Kwa sasa, SwahiliPot Hub Foundation inashirikiana na mashirika 57 kuvutia uwekezaji katika ukanda wa Pwani kupitia Baraza la Maendeleo ya Uchumi (Economic Development Council) linalopendekezwa, likiwa na lengo la kukuza biashara na kuongeza nafasi za ajira kwa vijana.
Waandalizi wanatarajia zaidi ya washiriki na wadau 10,000 kuhudhuria tamasha hilo la wiki moja la ubunifu.
Waandalizi wamesema Pwani Innovation Week 2026 itawaleta pamoja wadau kutoka serikalini, sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na taasisi za elimu ili kujenga mazingira yanayowawezesha vijana kubadili mawazo bunifu kuwa biashara endelevu. Kupitia ushirikiano huo, tukio hilo linatarajiwa kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Pwani, kuongeza uwekezaji na kufungua fursa zaidi za ajira kwa kizazi kijacho.
Comments
Post a Comment