KRA Yateketeza Bidhaa Haramu zenye Thamani ya Shilingi Milioni 218.


Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA), kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za kiusalama, imeteketeza bidhaa haramu zenye thamani ya Shilingi milioni 218 zilizokamatwa katika operesheni zilizofanyika jijini Nairobi na eneo la Pwani.

Uteketezaji huo ulifanyika kwa wakati mmoja katika kampuni ya Envirosafe Limited iliyoko EPZ Athi River, Nairobi, na katika eneo maalumu la Voi, Kaunti ya Taita Taveta. Bidhaa zilizoteketezwa zilijumuisha aina mbalimbali za bia, pombe kali na maji ya chupa ambazo zilikuwa zimekamatwa kupitia ukaguzi wa soko na operesheni za utekelezaji.

Uchunguzi umebaini kuwa bidhaa hizo zilikiuka sheria mbalimbali zinazodhibiti utengenezaji, uagizaji na uuzaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa. Baadhi ya ukiukaji huo ni pamoja na matumizi ya stempu bandia za ushuru, matumizi ya stempu zilizobadilishwa au ambazo hazijaamilishwa, uzalishaji haramu na wazalishaji wasio na leseni, pamoja na mbinu nyingine za kukwepa kulipa ushuru.

                                         

KRA imesema uteketezaji huo unaonyesha dhamira yake ya kulinda watumiaji, kulinda mapato ya serikali, kuhakikisha ushindani wa haki na kuvunja mitandao ya biashara haramu inayodhoofisha uchumi wa Kenya.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja Mkuu wa Walipa Kodi Wadogo na wa Kati, Michael Gichuki, amesema operesheni hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa KRA wa kulinda wafanyabiashara wanaofuata sheria na kudumisha uadilifu wa mfumo wa kodi nchini.

Amesema hatua hizo zinalenga kulinda afya, usalama na ustawi wa kiuchumi wa Wakenya, na si kuwaadhibu wafanyabiashara wanaofuata sheria. Akiongeza kuwa kuondoa biashara haramu kunasaidia kuunda mazingira salama na yenye ushindani wa haki kwa wafanyabiashara wanaolipa kodi ipasavyo.

                                         

Gichuki amebainisha kuwa biashara haramu ni tishio kubwa kwa uchumi wa Kenya kwani husababisha upotevu mkubwa wa mapato ya serikali na kuwaweka watumiaji katika hatari ya kutumia bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na usalama. Bidhaa nyingi bandia hutengenezwa katika mazingira yasiyo salama na bila usimamizi wa mamlaka husika.

Aidha, biashara haramu huwadhuru wazalishaji halali kwa kuleta ushindani usio wa haki, kuhatarisha ajira, kupunguza uwekezaji na kudhoofisha ukuaji wa viwanda. Kila bidhaa bandia inayouzwa humaanisha serikali inapoteza mapato ambayo yangetumika kuboresha huduma muhimu kama afya, elimu, miundombinu na usalama.

Mamalaka hiyo pia imewahimiza wafanyabiashara na wananchi kutumia Programu ya SOMA Label, inayopatikana bila malipo kupitia Apple App Store na Google Play Store, ili kuthibitisha uhalali wa stempu za ushuru kabla ya kununua bidhaa zinazotozwa ushuru.

                                     

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kupambana na biashara haramu, kulinda watumiaji, kuongeza mapato ya serikali, kuhakikisha ushindani wa haki na kuweka mazingira bora kwa biashara halali kwa mujibu wa sheria za kodi na kanuni za Kenya. 

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.