KENYA YAVUNJA REKODI YA DUNIA KWA UPANDAJI WA MIKOKO MOMBASA
Kenya imevunja Rekodi ya Dunia ya Guinness ya kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu wanaopanda miti ya mikoko kwa wakati mmoja, katika zoezi lililofanyika Jomvu, Kaunti ya Mombasa.
Jumla ya watu 4,196, wakiwemo maskauti, wanajamii na wahifadhi wa mazingira, walishiriki zoezi hilo. Kati yao, 4,124 walitimiza masharti ya Guinness World Records, na hivyo kuvuka kiwango cha awali cha washiriki 3,001.
Mafanikio hayo yanaunga mkono juhudi za serikali za kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032, huku yakilenga pia kurejesha mifumo ya ikolojia ya pwani na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Zoezi hilo liliongozwa na Huduma ya Misitu Nchini (KFS), Chama cha Maskauti Kenya na M-PESA Foundation, kwa kushirikiana na jamii pamoja na wadau wengine wa mazingira.
Tukio hilo limefanyika chini ya kaulimbiu “Mikoko yenye Afya kwa Uchumi Endelevu wa Buluu na Ustahimilivu wa Tabianchi,” likisisitiza umuhimu wa mikoko katika kulinda mazingira ya pwani, bioanuwai na maisha ya jamii.
Akizungumza baada ya rekodi hiyo kuthibitishwa, Naibu Mkuu Mwandamizi wa Wahifadhi wa Misitu katika Huduma ya Misitu Nchini (KFS), Clement Ng’oriareng, amesema zaidi ya skauti 5,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini walijitokeza kushiriki katika jaribio hilo la kihistoria.
Hata hivyo, baada ya mchakato wa uhakiki kufanywa kwa kuzingatia vigezo vya Guinness World Records, jumla ya washiriki 4,124 walitambuliwa rasmi, hatua iliyoiwezesha Kenya kuweka rekodi hiyo ya dunia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Skauti Kenya, Moses Danda, amesema mafanikio hayo ni ushahidi wa uwezo wa vijana wa Kenya kuongoza juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Danda akisema rekodi hiyo si tu mafanikio ya Kenya katika jukwaa la kimataifa, bali pia ni ishara ya uwezo wa vijana kuendesha kampeni za kimazingira zenye matokeo makubwa.
Akiongeza kuwa wanajivunia kuwa sehemu ya historia hiyo, akisisitiza kuwa zoezi hilo limeweka msingi muhimu wa kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Comments
Post a Comment