KAUNTI YA MOMBASA YAREJESHA MRADI WA "SKILLS MTAANI", ZAIDI YA TAASISI 400 ZA MAFUNZO ZASAJILIWA

       

Serikali ya Kaunti ya Mombasa imesajili zaidi ya taasisi 400 za mafunzo zitakazoshirikiana na kaunti hiyo katika utekelezaji wa mpango wa Elimu Scheme – Skills Mtaani, unaolenga kuwapa vijana ujuzi wa ufundi na kuwawezesha kujiajiri.

Mpango huo unalenga kuunganisha maelfu ya vijana wanaotafuta ujuzi na taasisi zenye uwezo wa kutoa mafunzo ya vitendo yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Kupitia mpango wa Skills Mtaani, vijana watanufaika na mafunzo katika fani mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa mikate na keki, urembo na henna, useremala, ushonaji na ubunifu wa mavazi, mabomba, ufundi wa umeme, uchomeleaji vyuma, ufundi wa magari, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), pamoja na taaluma nyingine.

Serikali ya kaunti imesema mpango huo ni uwekezaji katika kuwawezesha vijana kiuchumi, kuwapa fursa za kujitegemea na kuimarisha maendeleo ya Mombasa kwa kupeleka mafunzo karibu na jamii.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Sheriff Nassir, amesema kaunti ya Mombasa na Kenya Kwa jumla kuna idadi kubwa ya vijana wasio na ajira, hivyo kuna haja ya kuwapa ujuzi na fursa za kujipatia kipato. 

         

Amesema fedha za kutekeleza mpango wa Skills Mtaani tayari zimetengwa, na sasa juhudi zinaelekezwa katika kuharakisha utekelezaji wake ili vijana waanze kunufaika bila kuchelewa.

Abdulswamad amevitaka vyuo vya mafunzo ambavyo bado havijasajiliwa na serikali kukamilisha usajili wao haraka ili vipate nafasi ya kushiriki katika mradi huo. Akisema hatua hiyo pia itasaidia kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanafanyika kwa uwazi na uwajibikaji, kwa kuwa fedha zitaelekezwa kwa taasisi zinazotambuliwa rasmi na serikali. Ameongeza kuwa Idara ya Elimu ya Kaunti itazisaidia taasisi hizo kukamilisha taratibu zote za usajili.

Aidha, vyuo vitasaini mikataba na Serikali ya Kaunti ya Mombasa, huku vijana wakipewa nafasi ya kuchagua chuo na kozi wanazotaka kusomea. Maombi ya kujiunga na mpango huo yatafanywa kupitia mfumo wa mtandaoni, na Gavana Abdulswamad amesisitiza kuwa hakutakuwa na upendeleo katika mchakato wa uchaguzi. 

       

Gavana Abdulswamad Sharif Nassir amesema serikali ya kaunti itafuatilia mahudhurio ya wanafunzi watakaochaguliwa ili kuhakikisha wanahudhuria mafunzo na kupata ujuzi unaotarajiwa. Baada ya kuhitimu, baadhi ya wahitimu watasaidiwa kupata vifaa vya kuanzisha shughuli za kujiajiri kulingana na taaluma walizosomea, pamoja na kusaidiwa kutafuta nafasi za ajira ndani na nje ya nchi.

Gavana Nassir amewahimiza vijana kutuma maombi ya kujiunga na mradi huo, akisema utasaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kuongeza fursa za kujiajiri na kuwaepusha vijana na uhalifu pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

    


Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.