Kaunti ya Kilifi yazindua Kituo cha Uokozi kwa Manusura wa Dhuluma za Kijinsia


Kaunti ya Kilifi imezindua rasmi na kukabidhi Kituo cha Uokozi kilichopo eneo la Fumbini, Wadi ya Kibarani, ambacho kitatoa hifadhi salama kwa manusura wa dhuluma za kijinsia (GBV) kutoka maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.

Ujenzi wa kituo hicho umefadhiliwa na Children's Investment Fund Foundation (CIFF) na kutekelezwa na Shining Hope for Communities (SHOFCO) kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Kilifi. 
                  
Kituo hicho kitatoa huduma jumuishi ikiwemo ushauri nasaha, matibabu, malazi ya muda, mafunzo ya stadi za kujipatia kipato pamoja na maeneo ya watoto kucheza, ili kuwasaidia manusura kurejea katika maisha ya kawaida kwa heshima.

Kwa muda mrefu, manusura wengi wa dhuluma za kijinsia wamekuwa wakikosa mahali salama pa kuishi baada ya kuripoti visa vyao, hali iliyowalazimu kurejea kwa watu waliowafanyia ukatili au kuendelea kuishi katika mazingira hatarishi. Kituo hiki kinatarajiwa kutatua changamoto hiyo kwa kuwapatia hifadhi, ulinzi na huduma muhimu wanazohitaji.

Serikali ya Kaunti ya Kilifi ikiongozwa na naibu wake Flora Mbetsa Chibule imesisitiza kuwa kulinda makundi yaliyo hatarini ni jukumu la kila mmoja na imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha mifumo ya ulinzi wa jamii, kurejesha matumaini kwa manusura na kuhakikisha hakuna anayekabiliwa na dhuluma au migogoro akiwa peke yake.
                            
Kaunti ya Kilifi ni miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia visa vingi vya dhuluma za kijinsia, hivyo kituo hiki kinatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ulinzi na utoaji wa huduma kwa manusura.

Sehemu zilizokamilishwa katika kituo hicho ni pamoja na eneo la mapokezi, chumba cha muuguzi, vyumba vya ushauri nasaha, chumba cha mafunzo ya stadi, ukumbi wa chakula, jiko la kisasa, eneo la watoto kuchezea na vyoo. Miundombinu hiyo inaungana na bweni lililokuwepo awali ili kukifanya kituo hicho kuwa mahali kamili pa huduma kwa manusura.
                   

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.