Kampeni Zapamba Moto Kuelekea Uchaguzi wa Chama cha Dock Workers Union (DWU)

Huku ikiwa imesalia takriban mwezi mmoja Kwa uchaguzi wa chama Cha wafanyikazi wa Bandari(DWU) kampeni za kumtafuta katibu mkuu wa chama hicho zinaonekana kupamba moto.

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Bandari (DWU), Abubakar Mohammed Abdullahi, ameanza rasmi kampeni zake kuelekea uchaguzi wa chama utakaofanyika Agosti 13. Hadi sasa yeye ndiye mgombea pekee aliyetangaza nia ya kuwania nafasi ya Katibu Mkuu, akilenga kumrithi Simon Sang.

Katiba ya chama hicho DWU inaeleza kuwa anayewania nafasi ya Katibu Mkuu lazima asiwe mfanyakazi wa sasa wa mwajiri husika, na mfanyakazi yeyote anayetarajia kugombea analazimika kujiuzulu kwa kutoa notisi kwa mwajiri wake.

Abubakar ameongeza kasi ya kampeni kwa kutembelea maeneo mbalimbali ya makazi ya wanachama akitafuta uungwaji mkono kabla ya uchaguzi huo. 

Abubakar ni miongoni mwa viongozi wa chama waliowahi kufutwa kazi katika Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) pamoja na maafisa wengine wa chama kufuatia mgomo uliotajwa kuwa haramu wakati wa uongozi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa KPA, marehemu Francis Gichiri Ndua, chini ya utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Ajira na Mahusiano Kazini (ELRC) mjini Mombasa, ambapo Jaji Ocharo Kebira alibatilisha uchaguzi wa Suliman Otieno Owuor kuwa Katibu Mkuu wa DWU baada ya Simon Sang kuondolewa madarakani.

Mahakama iliamuru chama hicho DWU kufanya uchaguzi mpya ndani ya siku 60 kwa kuzingatia katiba ya chama na masharti ya sheria. Jaji Kebira alieleza kuwa uchaguzi uliofanyika Aprili ulikuwa batili na haukuzingatia taratibu za kikatiba.

Katika hukumu yake, jaji huyo alisema Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi alikiri kupokea malalamiko kadhaa kuhusu uchaguzi huo lakini aliendelea kuwasajili viongozi waliodaiwa kuchaguliwa.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa DWU, Mohammed Mwasera, ametangaza rasmi kuwa uchaguzi wa chama utafanyika Agosti 13. Katika taarifa iliyotumwa kwa wanachama wapatao 5,000, akiongeza kuwa uchaguzi huo unafanyika kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Juhudi za kupata maoni kutoka kwa Suliman Otieno Owuor pamoja na Salim Kumaka, ambaye yuko katika usimamizi wa chama, hazikufanikiwa baada ya simu zao kutopokelewa.

Wanachama wote wanaostahili kupiga kura wametakiwa kushiriki uchaguzi huo kwa amani na uwajibikaji, huku wakihimizwa kudumisha umoja, nidhamu na kuheshimu utawala wa sheria.

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.