Kalonzo Apinga Uuzaji wa Hisa za Serikali katika kampuni ya mawasiliano ya Safaricom.

Kiongozi wa Chama cha Wiper, Dkt. Stephen Kalonzo Musyoka, amepinga hatua ya Serikali kukamilisha uuzaji wa hisa zake za asilimia 15 katika kampuni ya Safaricom PLC kwa Vodacom, akisema mchakato huo umefanyika kabla ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi kuhusu kesi ya kikatiba inayopinga mauzo hayo.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari Kalonzo amesema Serikali iliharakisha kukamilisha shughuli hiyo mara baada ya Mahakama ya Rufaa kuondoa amri za kusimamisha mauzo hayo mnamo Juni 26, 2026, ilhali kesi ya msingi bado inasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu unaotarajiwa kutolewa ndani ya wiki mbili zijazo.

Kalonzo amesema Mahakama ya Rufaa haikuamua iwapo mauzo hayo yalikuwa halali, kama kulikuwa na ushirikishwaji wa kutosha wa wananchi au kama hisa za Safaricom zilithaminiwa kwa haki. Amesisitiza kuwa masuala hayo ya kikatiba bado hayajapatiwa uamuzi.

Aidha, ameeleza kuwa Safaricom ni rasilimali muhimu kwa taifa kutokana na nafasi yake katika uchumi wa kidijitali wa Kenya kupitia huduma ya M-Pesa, mawasiliano, biashara na utoaji wa huduma mbalimbali za umma.

Kwa mujibu wa Kalonzo, Serikali iliuza takribani hisa bilioni sita kwa bei ya Shilingi 34 kwa kila hisa, hatua iliyopunguza umiliki wake kutoka asilimia 35 hadi asilimia 20 na kuipa Vodacom umiliki wa takribani asilimia 55. Amedai kuwa ushahidi wa wataalamu uliowasilishwa mahakamani ulionyesha thamani halisi ya kila hisa kuwa karibu Shilingi 57.90.

Pia amehoji sababu za Serikali kuachana na mapato ya gawio ambayo yangepatikana katika siku chache zijazo badala ya kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kabla ya kukamilisha mauzo hayo.

Kalonzo amesema shughuli hiyo inaibua maswali kuhusu uwazi, uwajibikaji, uthamini wa mali ya umma na kuheshimu utawala wa sheria. Ameongeza kuwa ataendelea kutumia njia zote za kisheria na kikatiba kupinga mauzo hayo.

Vilevile ametoa wito kwa Wakenya kujisajili kama wapiga kura na kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 ili kuhakikisha viongozi wanawajibika kwa wananchi.

Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.