Idara ya Polisi yapokea Vifaa vya Kisasa Kuimarisha Utekelezaji wa Sheria za Trafiki
Shirika la Global Road Safety Partnership (GRSP), kupitia mpango wa Bloomberg Philanthropies Initiative for Global Road Safety (BIGRS), limekabidhi Huduma ya Kitaifa ya Polisi vifaa vya kisasa vya kuimarisha utekelezaji wa sheria dhidi ya uendeshaji wa magari chini ya ushawishi wa pombe na kupunguza ajali za mara Kwa mara barabarani.
Hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo maafisa wa Polisi wa Trafiki na kuimarisha utekelezaji wa sheria dhidi ya vihatarishi vikuu vya ajali, huku ikichangia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kuhusu usalama barabarani.
Mratibu wa BIGRS, Vipul Patel, amesema matumizi ya vifaa hivyo yatawezesha utekelezaji wa sheria unaozingatia ushahidi, kubaini madereva wanaoendesha wakiwa wamelewa na kusaidia kuokoa maisha kupitia usalama bora barabarani.
"Utekelezaji madhubuti wa sheria ni njia muhimu ya kupunguza ajali, vifo na majeraha barabarani. Makabidhiano haya ya vifaa yanaimarisha uwezo wa polisi na yanaonyesha dhamira yetu ya kushirikiana na wadau mbalimbali kujenga barabara salama nchini." Amesema Vipul
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na mashine 40 za kupima kiwango cha pombe mwilini (Dräger Alcotest 7000), vichapishi 20 vya Dräger Mobile Printer BT, koni 20 za kuelekeza magari na taa 20 za onyo kwa operesheni za ukaguzi barabarani.
Vifaa hivyo vinatarajiwa kuongeza ufanisi wa operesheni za polisi, kuimarisha utekelezaji wa sheria na kupunguza ajali, majeraha na vifo vinavyotokana na uendeshaji wa magari chini ya ushawishi wa pombe.
Comments
Post a Comment