Viongozi wa kiislamu wapongeza Kujumuishwa kwa Duksi na Madrasa Kwenye Mfumo wa Elimu Nchini.
Viongozi wa dini ya Kiislamu kutoka ukanda wa Pwani wamepongeza hatua ya Rais William Ruto ya kutaka mafunzo ya Madrasa na Duksi yajumuishwe katika mfumo wa elimu ya taifa, wakisema hatua hiyo itasaidia kuwajenga wanafunzi kiimani, kuwawezesha kuifahamu dini yao kwa kina kukuza hadhi ya madrasa na duksi.
Wakizungumza
na waandishi wa habari mjini Mombasa, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Pwani
Patriotic Religious Leaders, Sheikh Abu Qatada, viongozi hao wamesema hatua
hiyo itawasaidia wanafunzi kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kuwaepusha na
mienendo isiyokubalika kijamii.
Sheikh Abu
Qatada amesema kutambuliwa kwa masomo ya dini ya Kiislamu na serikali ni ishara
kwamba Rais Ruto ni kiongozi anayethamini dini zote na anatambua umuhimu wa
kumcha na kumtumikia Mungu.
Aidha, amesema
kuwa kujumuishwa kwa mafunzo ya Madrasa na Duksi kutatoa fursa kwa walimu
waliohitimu katika masomo hayo kupata ajira katika shule za umma na za
kibinafsi, jambo litakalowawezesha kujikimu kimaisha.
"Tunamshukuru
sana Rais kwa kutukumbuka sisi kama jamii ya Waislamu katika taifa hili.
Tunampongeza kwa hatua aliyochukua ya kuhakikisha elimu ya Madrasa na Duksi
inatambuliwa rasmi katika mfumo wa elimu wa serikali," alisema.
Kwa upande
wake, Katibu wa Chuo cha Mafunzo ya Kiislamu cha Sheikh Siraj Rahman, Salim
Kifaru, amesema tayari taasisi yao imeanzisha mfumo wa mafunzo unaotambulika
kitaifa, ambao utawawezesha wahitimu kupata ajira kupitia vyeti
vinavyotambuliwa.
Amesema
kauli ya Rais Ruto inafungua njia kwa Madrasa na Duksi kuwa na mtaala unaoendana
na mfumo wa elimu nchini, hali itakayowezesha utoaji wa vyeti vinavyotambuliwa
na Wizara ya Elimu.
"Hii ni
tunu kubwa ambayo Rais Ruto ametupatia sisi Waislamu, na tuna wajibu wa
kushirikiana na serikali kuhakikisha hatua hii inatekelezwa kwa manufaa ya
wanafunzi na jamii kwa ujumla," alisema.
Naye
Mwenyekiti wa Muungano wa Maimamu na Walimu wa Madrasa wa Kilifi Kusini, Sheikh
Hassan Mubarak, amesema hatua hiyo ni ya kihistoria na ya maendeleo kwa kuwa
itahakikisha ushirikishwaji na upatikanaji sawa wa elimu kwa watoto wote bila
ubaguzi.
Akitoa wito
kwa Wizara ya Elimu kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa kikamilifu ili watoto
wote waweze kupata elimu bora na inayotambuliwa rasmi.
"Tunashukuru
na kupongeza uamuzi huu wa busara uliofanyika kwa wakati mwafaka. Ni hatua
yenye manufaa makubwa kwa taifa na kwa vizazi vya sasa na vijavyo,"
alisema.

.jpeg)

Comments
Post a Comment