Mombasa yaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Baiskeli; Wadau Washinikiza Uimarishaji wa miundombinu kurahisisha uchukuzi.

                                                                 


Mamia ya waendesha baiskeli walijumuika na viongozi wa Kaunti ya Mombasa pamoja na wadau wa sekta ya usafiri kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Baiskeli huku kaunti hiyo ikithibitisha dhamira yake ya kuendeleza miundombinu salama ya waendesha baiskeli na kuhimiza matumizi ya usafiri endelevu.

Maadhimisho hayo yalifanyika wakati ambapo Mombasa inaendelea kushuhudia maendeleo makubwa katika ujenzi wa njia maalum za waendesha baiskeli, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa magari, kuboresha afya ya wananchi na kupunguza uzalishaji wa hewa kaa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo naibu Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Francis Thoya, amesema matumizi ya baiskeli yanazidi kuwa mtindo wa maisha na suluhisho la changamoto za usafiri zinazokabili kaunti hiyo.

                                                  

Ameweka wazi  kuwa serikali ya kaunti kwa ushirikiano na wadau mbalimbali tayari imeanza kupanua miundombinu ya baiskeli kutoka Barabara ya Links kuelekea katikati ya jiji ili kuwahamasisha wananchi kutumia zaidi usafiri huo.

Thoya pia amesisitiza umuhimu wa baiskeli katika kulinda mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kutoka kwa magari.

“Mombasa ni kaunti ndogo zaidi nchini Kenya lakini inaendelea kukua kwa kasi. Eneo ni finyu na msongamano wa magari unaongezeka kila siku. Ni wakati wa wananchi kuanza kufikiria njia mbadala za usafiri,ambayo pia itasaidia kulinda mazingira yetu,”

Mkurugenzi Mkuu wa EBee Africa, Maarten Fonteijn, alisema siku hiyo haikuwa tu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Baiskeli bali pia kusherehekea kukamilika kwa awamu ya kwanza ya njia ya waendesha baiskeli katika kaunti hiyo.

                                                       

Alibainisha kuwa matumizi ya baiskeli ni suluhisho mojawapo la changamoto ya msongamano wa magari mjini Mombasa kwani yanawawezesha wananchi kufika maeneo yao kwa haraka huku wakiboresha afya zao.

"Tunafurahia kukamilika Kwa njia ya baiskeli itasaidia pakubwa pia katika kupunguza msongamani wa magari"

                                                                

Kwa upande wake, mkurugenzi wa Kanda wa ITDP Africa Claire Birungi amesema idadi kubwa ya watu waliojitokeza kushiriki hafla hiyo ni ishara kwamba wananchi wamekubali matumizi ya baiskeli na sasa kilichobaki ni kuimarisha miundombinu salama ya waendesha baiskeli.

 Aliongeza kuwa ujenzi wa njia ya baiskeli katika Barabara ya Links tayari umeanza, ambapo takribani kilomita nne zimejengwa na mipango ipo ya kuipanua hadi kilomita nane.

“ Zaidi ya waendesha baiskeli 200 wamejitokeza kuunga mkono shughuli hii. Tunahitaji kuendelea kuwekeza katika miundombinu salama ya baiskeli inayounganishwa na mifumo mingine ya usafiri wa umma,”

                                                         

Wadau hao walieleza kuwa miundombinu bora ya baiskeli itasaidia watoto kusafiri kwa usalama, kukuza biashara kwa kurahisisha ufikiaji wa wateja na kuwapa wananchi njia nafuu na salama ya usafiri.

Kwa upande wake meneja wa programu Global Designing Cities Initiative, Regatu  Solomon amesema Mombasa ni miongoni mwa miji kumi duniani iliyochaguliwa kati ya miji 275 kufaidika na mpango wa Bloomberg Initiative for Cycling Infrastructure (BICI), unaosaidia miji kujenga miundombinu salama na jumuishi ya waendesha baiskeli.

                                                         




“Tunatoa msaada wa kiufundi na kifedha ili kusaidia Mombasa kutekeleza miundombinu salama ya waendesha baiskeli kwa manufaa ya watumiaji wote wa barabara,” alisema.

Mombasa inaelekea kuwa miongoni mwa miji inayoongoza katika kuhamasisha matumizi ya baiskeli kama njia salama, nafuu na endelevu ya usafiri.


Comments

Popular posts from this blog

Viongozi wa Kidini PPRL Waunga Mkono Agizo la wizara ya elimu la Ratiba ya Masomo Shuleni

Mbunge Feisal Bader Atuhumiwa Kuzuia Msambweni Talent Show Kufanyika Mvindeni Youth Centre.

Kaunti ya Wajir yaandaa Sherehe za Madaraka Day kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru.