Kenya yathibitisha Kuimarisha Usalama wa Baharini Katika Mkutano wa 4 wa Kamati ya Uongozi ya IORIS,Mombasa.
Kenya imethibitisha dhamira yake ya kuimarisha usalama wa baharini na ushirikiano wa kimataifa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 4 wa Kamati ya Uongozi ya Jukwaa la Indo-Pacific Regional Information Sharing Platform (IORIS) unaofanyika Mombasa.
Washiriki wanatarajiwa kujadili changamoto mbalimbali za
usalama wa baharini ikiwemo uharamia, wizi wa kutumia silaha baharini, uvuvi
haramu usioripotiwa na usiodhibitiwa (IUU), pamoja na utupaji wa taka na
kemikali hatari katika mazingira ya bahari.
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amesema kuwa
bahari imekuwa mhimili muhimu wa biashara ya kimataifa kwa karne nyingi,
zikichangia ukuaji wa uchumi wa mataifa mbalimbali. Hata hivyo, migogoro
inayoendelea katika Mashariki ya Kati imeonyesha jinsi usumbufu wa njia za
usafiri wa baharini unavyoweza kuathiri uchumi wa dunia na maisha ya watu
wengi.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa na ubia kama ule
unaoendelezwa kupitia mkutano huo ni muhimu katika kulinda rasilimali za pamoja
za baharini na kuhakikisha biashara ya kimataifa inaendelea bila vikwazo.
Kenya pia ilitoa shukrani kwa Umoja wa Ulaya kwa ushirikiano
wake wa muda mrefu katika kuimarisha usalama wa baharini kupitia miradi ya
kujenga uwezo na kutoa suluhu za vitendo dhidi ya vitisho vya baharini.
Kupitia mpango wa CRIMARIO, taasisi mbalimbali za Kenya
zikiwemo Jeshi la Wanamaji la Kenya, Huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya,
Mamlaka ya Bandari Kenya, Mamlaka ya Bahari Kenya pamoja na Kamati ya Kuratibu
Operesheni za Udhibiti wa Mipaka (BCOCC), zimekuwa wanachama hai wa jamii ya
IORIS.
Jukwaa la IORIS limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha
mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa muhimu kati ya taasisi za usalama wa
baharini, hivyo kuimarisha ufuatiliaji wa maeneo ya bahari na usalama wa njia
za usafiri wa majini.
Maswala mengine yaliyo angaziwa ni maendeleo ya programu ya
simu ya Usalama Baharini, iliyobuniwa kwa ushirikiano kati ya Huduma ya
Walinzi wa Pwani ya Kenya na CRIMARIO. Programu hiyo imeunganishwa na mfumo wa
IORIS na inawawezesha wavuvi pamoja na watumiaji wengine wa bahari kupata
taarifa muhimu za usalama na tahadhari kwa wakati.
Maafisa hao walisema teknolojia hiyo imeongeza uwezo wa
Huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya kufuatilia shughuli baharini na kutoa mwitikio
wa haraka dhidi ya vitisho vya kiusalama.
Kenya imesisitiza kuwa iko tayari kuendelea kushirikiana na
mataifa na wadau wengine katika kupambana na vitisho vya baharini na
kuhakikisha uhuru wa usafiri wa majini unaendelea kulindwa.
Washiriki wa mkutano huo wamehimizwa kutumia fursa hiyo
kutathmini mafanikio yaliyopita, kujifunza kutokana na changamoto
zilizojitokeza na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ushirikiano wa
baharini siku zijazo.
Mkutano huo wa siku tatu umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya
mpango wa Critical Maritime Routes Indo-Pacific (CRIMARIO) unaofadhiliwa na
Umoja wa Ulaya na Huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya (KCGS) na umewaleta
pamoja wadau wa sekta ya bahari kujadili njia za kuimarisha usalama wa bahari
na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Mkutano huo unatarajiwa kuhitimishwa kwa mapendekezo
yatakayosaidia kuimarisha utawala wa bahari, ushirikiano wa kiusalama na
ubadilishanaji wa taarifa katika ukanda wa Indo-Pacific na kwingineko duniani.





Comments
Post a Comment