Huku maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 yakizidi
kushika kasi, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Mohamed Nur, ametoa onyo kali kwa
wanasiasa wanaotumia magenge ya wahuni na vijana kuvuruga mikutano ya kisiasa
ya wapinzani wao au kujifanya maafisa wa usalama.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Madaraka
yaliyofanyika katika Uwanja wa Bilima, Kaunti Ndogo ya Kisauni,Nur amesema vyombo vya usalama vinafuatilia kwa
karibu shughuli za kisiasa na havitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote
atakayekiuka sheria.
Kamishna huyo alisisitiza kuwa kudumisha amani, utulivu na
usalama ni jukumu la kila mwananchi, akiongeza kuwa hakuna mtu atakayelindwa
kutokana na hatua za kisheria kwa misingi ya hadhi au cheo chake Kwa jamii,
ushawishi wa kisiasa au chama anachokiunga mkono.
Nur alieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la visa ambapo
baadhi ya wanasiasa wanadaiwa kuwatumia vijana na makundi ya wahuni kusababisha
vurugu katika mikutano ya kisiasa, akisema tabia hiyo inahatarisha amani,
demokrasia na mshikamano wa kitaifa.
Aliwataka viongozi wa kisiasa kuendesha shughuli zao kwa
uwajibikaji na kuheshimu haki za wapinzani wao kufanya mikutano na kuwasiliana
na wafuasi wao bila kuingiliwa.
Aidha, aliwashauri wanasiasa wanaohitaji ulinzi wakati wa
shughuli zao kutafuta huduma rasmi za usalama kutoka kwa Jeshi la Polisi badala
ya kutegemea wahuni au makundi ambayo hayajaidhinishwa.
Kamishna huyo pia aliwataka wakazi wa Mombasa kushirikiana
na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaopanga au kushiriki
katika vitendo vya uhalifu na vurugu vinavyoweza kuvuruga mikutano ya umma.
Kauli zake zinajiri wakati shughuli za kisiasa nchini
zinaendelea kuongezeka kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, huku serikali na
vyombo vya usalama vikiahidi kuhakikisha kuwa kampeni na mikutano ya kisiasa
inafanyika kwa amani, utulivu na kwa kuzingatia sheria za nchi.
Comments
Post a Comment