Viongozi kutoka kaunti ya Mombasa wajitokeza kumtetea Hassan Omar Sarai.
Baadhi ya viongozi na wakazi wa Kaunti ya Mombasa wanaendelea kujitokeza kumtetea Katibu Mkuu wa Chama cha UDA, Hassan Omar Sarai, kufuatia semi zake zilizoibua utata.
Hii ni baada baadhi ya viongozi kutoka eneo la Mlima
Kenya kushinikiza Katibu mkuu huyo wa UDA ajiuzulu kutoka wadhifa wake kwa
madai ya semi zake zinachochea ukabila.
Wakiongozwa na mwanaharakati wa kisiasa Said Twaha
wamesema kuwa kauli za Sarai zilikuwa zinalenga kutetea haki za wakazi wa Pwani
waliopokonywa mashamba yao, na wala hazikulenga kuchochea jamii yoyote kama
inavyodaiwa na baadhi ya viongozi hao.
Twaha amesema wataendelea kusimama kidete na Katibu
Mkuu huyo wa UDA kwa kuwa amekuwa nguzo muhimu ya umoja na mshikamano wa amani
katika eneo la Pwani.
Aidha, amemhakikishia Rais kuwa watafanya kila
juhudi kuhakikisha chama cha UDA kinapata asilimia 100 ya kura katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2027.
“Hassan Sarai ameongea kutetea watu wake WA pwani na
hakuchochea ukabila,sisi tumeishi Kwa amani tangu jadi. Tunamwambia Rais
tunataka Hassan Sarai asibanduliwe katika wadhafa wake”.
Kwa upande wake, mmoja wa viongozi wa vijana kutoka Kaunti ya Mombasa, Suleiman Hassan, amesema vijana wataendelea kumuunga mkono Sarai na hawatakubali abanduliwe katika wadhifa huo.
Amesema Sarai aliteuliwa na Rais kwa
lengo la kuimarisha ujumuishaji wa jamii mbalimbali serikalini na kwamba
ameendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
“Maneno ya Sarai kujiuzulu tumekataa.katika UDA viti
vimegawanywa kuleta ujumuishwaji WA Kila jamii,kutaka kumtoa ni kutuonea”.
Naye Mohamed Yere, mmoja wa viongozi kutoka jamii ya Wasomali katika Kaunti ya Mombasa, amesema kuwa iwapo Sarai ataondolewa katika nafasi yake, wao pia watajiondoa ndani ya chama hicho.
Amekemea vikali madai kwamba Sarai
anachochea ukabila, akisema amekuwa kinara wa kuunganisha jamii tofauti.
“Sisi kama jamii ya Wasomali tumekataa na akitolewa
tutatoka na yeye. Sarai hana ukabila wenye ukabila wabaki na ukabila wao”.
Joyce Wairimu amesema kuwa wakazi wa Mombasa
wameishi kwa amani na mshikamano kwa miaka mingi bila ubaguzi wa kikabila, na
kwamba Sarai amekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha umoja huo.
Kwa upande wake, Halima Omar amesema Sarai ni
kiongozi anayeheshimu na kuthamini jamii zote bila kujali kabila, na kwamba
amekuwa akifanya kazi kwa misingi ya usawa na ujumuishaji.

.jpeg)
Comments
Post a Comment